Na: Mwandishi Wetu – Moshi, Kilimanjaro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amemuagiza mkandarasi anayejenga Kiwanda cha kuchakata bidhaa za Ngozi cha Karanga (Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd) kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua ya pili ya ujenzi wa mradi huo (LOT 2).
Waziri Mhagama alitoa kauli hiyo Agosti 18, 2021 Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya kiwanda hicho cha kutengeneza viatu sambamba na kukagua ujenzi wa awamu ya pili ya kiwanda cha kuchakata ngozi.
Alieleza kuwa, kazi nzuri ilifanyika katika hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi (LOT 1) ambayo ilihusisha ujenzi wa kiwanda cha viatu yaani majengo ya ukataji na ushonaji, umaliziaji ghala na nyumba ya mitambo ya umeme ilikamilika kwa wakati na kampuni hiyo imeanza kutumia baadhi ya majengo kwa ajili ya ofisi.
“Hatua ya pili ya ujenzi wa mradi (LOT 2) ni muhimu sana kwa kuwa kiwanda hicho cha kuchakata ngozi kitakuwa fungamanishi na kiwanda ambacho kimeshakalika katika hatua ya kwanza, hivyo ni vyema Mkandarasi ahakikishe anakamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuchakata ngozi, karakana, maabara, bwalo la chakula kwa ajili ya wafanyakazi wa kiwanda, nyumba ya mitambo ya umeme (Power House), tanki la maji na mtambo wa kutibu maji taka ya kiwandani,” alisema Waziri Mhagama.
Alifafanua kuwa, kukamilika kwa kiwanda hicho cha kuchakata ngozi kutasaidia kuondoa tatizo la kupata ngozi zenye ubora na ngozi itakayozalishwa katika kiwanda hicho itaweza kuuzwa kwenye viwanda vidogo vidogo vilivyopo nchini pamoja nan je ya nchi.
Aliongeza kuwa, kazi zote za msingi katika kiwanda hicho zikamilishwe kwa wakati ili wataalamu kutoka nchi ya Italia wakiwasili kwa ajili ya kufunga mitambo wakute hatua zote katika kiwanda cha kuchakata ngozi ziwezimekamilishwa.
“Uwekezaji huu utaleta tija ndani ya taifa na kadri kiwanda hiki kinavyojengwa kitakuwa kiwanda kikubwa Afrika Mashariki na Afrika ya kati,” alisema
Sambamba na hayo, Waziri Mhagama alizitaka taasisi zote zinazohusika katika kusimamia mradi huo ikiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Jeshi la Magereza Nchini, Shirika la Maendeleo ya Utafiti wa Viwanda Tanzania (TIRDO) pamoja na Mkandarasi ili kuufanya mradi huo ukamilike kwa wakati.
“Ni vyema mkakutana kwa pamoja na kuweka vitu vyote sawa kama wahusika katika mradi huu ili kila mmoja wenu aweze kutekeleza wajibu wake. Pia nitakapotoka hapa leo nitakutana na kuzungumza na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wanaohusika katika mradi huu ili tuwe na uelewa wa pamoja katika kuhakikisha ujenzi wa mradi wa kimkakati uliopangwa kutekelezwa na Serikali unakamilika kwa wakati na kuweza kuleta tija iliyokusudiwa,” alisema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama amepongeza njia bora inayotumika katika kukuza masoko ya bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda hicho cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd ikiwa ni pamoja na kuweza kuuza bidhaa nje ya nchi.
“Nimefurashwa na maendeleo ya kiwanda hasa upande wa masoko kwa kuweza kukuza soko la bidhaa zinazozalishwa kiwanda hapa, mmefanikiwa kuuza katika nchi jirani ikiwemo Kenya na maeneo mengine ndani ya Afrika Masharaki sasa ongezeni wigo katika soko la SADC na maeneo mengine zaidi,” alisema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), CPA. Hosea Kashimba alisema kuwa ofisi yake itaendelea na taratibu zote muhimu zinazohitajika katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na muda uliopagwa.
Naye, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini (TSSA), Bw. Meshack Bandawe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kusimamia vizuri uchumi wa nchi hususan katika eneo la viwanda ili kwenda sambamba na dira ya taifa itakayotutoa katika uchumi wa kati na kwenda uchumi wa juu.
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho cha Kilimanjaro International Leather Industries Co. Ltd Bw. Masoud Omari alisema uongozi wa kiwanda hicho umepokea maelekezo yote yaliyotolewa na wamejipanga kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati.