Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kalemani Awatoa Hofu Wananchi Kuhusu Matumizi ya REA
Sep 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Veronica Simba – Mara

Wananchi wametakiwa kuondoa hofu kuwa umeme unaosambazwa vijijini kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ni mdogo usioweza kutumika kwa shughuli kubwa za kibiashara kwani si kweli, kwakuwa umeme huo una nguvu sawa na umeme mwingine na unaweza kutumika kwa matumizi yote ikiwemo viwanda.

Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, wakati akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali katika Wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara, pamoja na Bariadi mkoani Simiyu, Septemba 19, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.

Waziri Kalemani alisema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa na hofu kuwa huenda umeme huo ambao Serikali inausambaza vijijini  ni mdogo usioweza kuendesha shughuli kubwa za kibiashara zinazohitaji umeme mkubwa.

“Naomba niwahakikishie kwamba, umeme wa REA hautumiki kwa ajili ya kuwashia taa tu, bali ni umeme kama ulivyo umeme mwingine na una uwezo wa kutumika katika shughuli zote hata kuendeshea viwanda vikubwa.”

Akieleza zaidi, Waziri alifafanua kuwa, lengo la Serikali kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa REA ni kuhakikisha umeme huo mbali na kutumika kwa matumizi madogomadogo ya kawaida, utumike zaidi kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo na hata vikubwa, ili kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Alisema kuwa, katika kuwezesha uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria viwanda hivyo vianzishwe vijijini ambako ndiko kwenye rasilimali nyingi, na kwamba Serikali inatambua kuwa umeme ndiyo ‘injini’ ya uchumi wa viwanda; hivyo ni lazima upelekwe umeme unaoweza kukidhi matakwa hayo.

Aidha, Waziri kalemani alisema sababu nyingine ya Serikali kupeleka umeme vijijini ili kuwezesha shughuli kubwa za kiuchumi ni ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya watu wengi hususan vijana kukimbilia mijini ili kujitafutia maisha. “Tunataka vijana, ambao ndiyo nguvu-kazi ya Taifa wabaki katika vijiji vyao na kufanya shughuli za maendeleo wakiwa hapahapa.”

Waziri Kalemani aliwahamasisha wananchi, wakiwemo wanawake na vijana, kuutumia umeme ambao Serikali inawapelekea kwa shughuli mbalimbali za ujasiriamali kama vile saluni, kuchomelea vyuma, mashine za kusaga na kukoboa nafaka na shughuli nyingine mbalimbali za kimaendeleo.

Vilevile, alihamasisha uongozi wa halmashauri za Wilaya, Vijiji na Kata, kuhakikisha taasisi mbalimbali za umma zinaunganishiwa nishati hiyo muhimu, kwa kushirikiana na timu ya wataalam kutoka TANESCO, REA na Wakandarasi katika kubainisha maeneo kulipo na taasisi husika.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani  aliwasha rasmi umeme katika Majengo ya Maabara na Upasuaji ya Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Vijiji vya Bukama na Nyangere wilayani Bunda, Shule ya Sekondari Itilima na Kijiji cha Luguru vilivyopo wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

Pia, alizungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na wa Kijiji cha Salama ‘A’ kilichopo Bunda, ambapo Mradi wa Ujazilizi wa Umeme (Densification) unatekelezwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi