* Awasha umeme Unangwa na Changarawe
Na Veronica Simba – Songea
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa onyo kali kwa wanaohujumu miundombinu ya umeme nchini kote akisema serikali imedhamiria kupambana nao na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika.
Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti jana, Aprili 3, 2019 akiwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma, Wilaya ya Songea ambapo aliviwashia umeme vijiji vya Unangwa na Changarawe pamoja na kuzungumza na wananchi.
Aliwaomba wananchi kuwa wazalendo kwa kulinda miundombinu ya umeme iliyo katika maeneo yao na kuwafichua wale wanaoihujumu ili wachukuliwe hatua kwani wanarudisha nyuma jitihada za serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumzia tukio la kuhujumu miundombinu ya umeme lililotokea hivi karibuni eneo la Mlandizi na kusababisha ukosefu wa umeme kwa mikoa na wilaya kadhaa, hususani Dar es Salaam; Waziri alisema ameunda timu maalumu kuchunguza waliohusika ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alitoa maagizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu utaratibu wanaopaswa kuufuata ili waunganishiwe umeme.
Alisema, katika ziara ambazo amekuwa akifanya maeneo mbalimbali nchini, amegundua wananchi wengi bado hawana uelewa wa utaratibu sahihi wanaopaswa kufanya ili wapate umeme hali inayosababisha wengi wao walalamike kutopewa huduma hiyo muhimu, wakidhani hawatendewi haki.
“Sehemu nyingi nimekutana na malalamiko ya wananchi wakidai hawajaunganishiwa umeme lakini ukifuatilia unabaini hawajalipia ndiyo maana hawajapatiwa huduma. TANESCO waelimisheni wananchi waelewe,” alisisitiza.
Akifafanua zaidi, alisema hata baadhi ya taasisi mbalimbali zikiwemo shule, vituo vya afya, masoko, miradi ya maji na nyinginezo, hususani zilizoko vijijini, kumekuwa na malalamiko ya kutounganishiwa umeme lakini baada ya kufuatilia imebainika wengi wao hawajalipia ndiyo maana hawajaunganishiwa.
Sambamba na kuhamasisha wananchi kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme, Waziri pia aliwahamasisha wale wenye nyumba zenye vyumba vichache watumie vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) badala ya kutandaza nyaya (wiring) ili kupunguza gharama.
Alisema serikali imetoa vifaa hivyo 250 bure kwa kila eneo ambako wakandarasi wa umeme vijijini wanaendelea kuunganisha wananchi na kwamba idadi hiyo ikiisha vitauzwa kwa gharama ndogo ya shilingi 36,000 tu.
Katika ziara hiyo pia, Waziri alikagua miundombinu mbalimbali ya Mradi mkubwa wa umeme wa Makambako – Songea unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, Jumamosi ya Aprili 6, mwaka huu mjini Songea.
Waziri alifuatana na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO na REA.