Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kalemani Amvua Cheo Meneja wa Tanesco Bukombe
Sep 15, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_46863" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa Bukombe mkoani Geita, alipokuwa katika ziara ya kazi, Septemba 14, 2019.[/caption]

Na Veronica Simba - Geita

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumwondolea wadhifa wake, aliyekuwa Meneja wa shirika hilo wilayani Bukombe, Thadei Mapunda kutokana na utendaji kazi usioridhisha na kuteua Meneja mwingine kuanzia Septemba 14, 2019.

Alitoa maelekezo hayo jana, Septemba 14 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo.

“Mkurugenzi Mtendaji Makao Makuu, sijaridhishwa na utendaji kazi wa Meneja wa Wilaya hii. Naagiza muweke pembeni sasa hivi. Huyu siyo Meneja wa hapa kuanzia leo,” alielekeza Waziri.

[caption id="attachment_46862" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria uwashaji wa umeme Kijiji cha Igulwa, wilayani Bukombe, Septemba 14, 2019. Kulia kwake ni Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini Doto Biteko na kushoto kwake ni bibi mwenye nyumba iliyowashiwa umeme, Elizabeth Herman.[/caption]

Akizungumza na wananchi wa Bukombe, katika uwanja wa stendi ya zamani, Waziri Kalemani aliwaeleza kuwa uamuzi wake wa kumwondoa Meneja huyo unatokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa maeneo mbalimbali wilayani humo kutokupatiwa huduma ya umeme pasipo sababu za msingi.

“Nimepita Kapela, kuna nyumba nzuri, kubwa lakini hazina umeme. Ni masikitiko makubwa sana, Halafu namuuliza Meneja hizi nguzo zimechimbiwa lini; ananiambia mwezi uliopita wakati nauona ni udongo wa leo na jana.”

Katika hatua nyingine, Waziri alisisitiza kuwa gharama za kuunganishiwa umeme vijijini ni shilingi 27,000 na kuwaonya mameneja wa TANESCO nchi nzima kutowalipisha nguzo wananchi vijijini.

Aidha, kabla ya kwenda kuzungumza na wananchi hao, Waziri alipita maeneo mbalimbali kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, ambayo ni pamoja na soko kuu na kuagiza pafungwe transfoma na maduka yaliyopo eneo hilo yaunganishiwe umeme ndani ya siku moja.

[caption id="attachment_46864" align="aligncenter" width="750"] Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, akizungumza na wananchi, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (meza kuu) katika eneo hilo, Septemba 14, 2019.[/caption]

Vilevile, Waziri alitoa siku 30 kwa mameneja wa TANESCO wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa, kwa kushirikiana na mkandarasi, kuhakikisha maeneo ya Nifa, Majengo, Kerezia, Maghorofani, Stendi Kuu na Stendi ya Mabasi yawe yamewashiwa umeme ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bukombe ambaye pia ni Waziri wa Madini, Doto Biteko, alimshukuru na kumpongeza Waziri Kalemani kwa kazi kubwa anayoifanya.

[caption id="attachment_46865" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Mkumba, akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wilayani humo, Septemba 14, 2019.[/caption]

“Ninao ujasiri na imani kwamba, chini ya Dkt Kalemani, wananchi wa Bukombe, maswali yenu ya umeme yamepata majibu leo,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Mkumba, pamoja na kumpongeza Waziri Kalemani na Mbunge wa eneo husika Doto Biteko kwa kuchukua hatua za kushughulikia matatizo ya umeme kwa wananchi husika mapema; aliahidi kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri.

[caption id="attachment_46866" align="aligncenter" width="750"] Umati wa wananchi wa kijiji cha Nakayondwa wilayani Chato, Mkoa wa Geita, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), aliposimama kuzungumza nao akitokea Wilaya ya Bukombe katika ziara ya kazi, Septemba 14, 2019.[/caption]

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi