Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Kairuki akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini.
Apr 10, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na. Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Dan Kazungu mapema hii leo Aprili 10, 2019 katika ofisi zake Jijini Dodoma.

Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa kujadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ambavyo Kenya inavyoweza kushirikiana na Tanzania katika masuala ya uwekezaji ambapo wako wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika masuala ya uchakataji wa korosho, kuongeza uwekezaji katika kilimo cha chai kwa mikoa miwili ya Iringa na Njombe, kuwekeza katika uchakataji wa mazao hayo pamoja na uwekezaji katika sekta ya nishati.

“Tumelenga kuona namna ambavyo tunaweza kuwekeza nchini Tanzania hususan katika maeneo ya vipaumbele ikiwemo kilimo cha kuchakata korosho, chai pamoja na kuwekeza kwenye nishati ya umeme,”alieleza Balozi Kazungu

Sambamba na hilo Mhe. Kairuki na Mhe. Kazungu wamekusudia kuandaa mkutano wa masuala ya uwekezaji kati ya mwezi Mei na Juni 2019 utakaofanyika nchini Tanzania.

Aidha Balozi huyo aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa nchi ya Tanzania kwa kuzingatia vivutio vilivyopo pamoja na mazingira bora ya biashara na uwekezaji yaliyopo nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu) anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki aliwashukuru wawekezaji wa Kenya kwa nia yao ya kuwekeza nchini na kuahidi kuwapa ushirikiano wake na wa Serikali wakati wote watakapokuwa tayari na itakapohitajika.

Pamoja na shukrani hizo Waziri Kairuki alimuomba Balozi huyo kuzingatia fursa za vipaumbele za uwekezaji ikiwa ni pamoja na viwanda vya nguo, mafuta ya kula, uchakataji wa mazao ya mifugo, vifungashio, pembejeo za kilimo hususan mbegu bora kwa ajili ya mazao ya kimkakati na mbolea, viwanda vya madawa na vifaa tiba, kemikali na fursa zinginezo.

“Niwashukuru sana wawekezaji na wafanyabiashara wa Kenya kwa kuonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kuzingatia Tanzania ina mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, pamoja na mifumo mizuri inayovutia wawekezaji nchini,”alisisitiza Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alibainisha miongoni mwa jitihada za Serikali kujenga mazingira wezeshi kwa uwekezaji ambapo alieleza kwamba Serikali itaendelea kuboresha na kutatua changamoto zilizopo ili kuhakikisha Tanzania inakuwa Kitovu cha Uwekezaji wa Mitaji katika nchi za Kusini Mwa Jangwa la Sahara na Afrika Mashariki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi