Serikali imezielekeza Mamlaka za udhibiti zilizopo kwenye maeneo ya mipaka mbalimbali nchini kuhakikisha shehena yoyote ya taka hatarishi inayosafirishwa nje ya nchi au inayoingizwa nchini na kupitishwa kwenye mipaka ya nchi inakuwa na kibali kilichotolewa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za usafirishaji wa chuma chakavu aina ya chuma dongo (Cast Iron) nje ya nchi licha ya kutokutolewa kwa kibali hicho tangu Machi hadi Septemba, 2023.
Akizungumza leo Septemba 22, 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kupitia usafirishaji wa taka hizo nje ya nchi, zipo tozo, ada na kodi zinazopaswa kulipwa, hivyo ukwepaji huo husababisha Serikali kukosa mapato.
Ameongeza kuwa suala hili husababisha kupungua kwa fursa za ajira kwenye viwanda vinavyotumia chuma chakavu aina ya chuma dongo kama malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nondo.
“Ikumbukwe kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo mkubwa katika suala la uwekezaji wa viwanda vya ndani kwa lengo la kuzalisha ajira na kukuza uchumi hivyo usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za chuma chakavu ikiwemo chuma dongo (Caste Iron) nje ya nchi kiholela na usiofuata utaratibu unaweza kusababisha upungufu wa malighafi kwenye viwanda vinavyotumia malighafi za aina hiyo hapa nchini kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo nondo na bomba za chuma,”.
“Upungufu wa malighafi unaweza kusababisha kupungua kwa ajira kwa vijana wanaofanya kazi katika viwanda vyetu vya ndani pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa aina ya nondo na bomba za chuma ambazo zinatumika sana katika shughuli za ujenzi wa nyumba za wananchi, ujenzi wa majengo ya serikali na sekta binafsi, pamoja na ujenzi wa wamiundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, reli, madaraja, na mabwawa ya kuzalisha umeme,” amesema Dkt. Jafo.
Hivyo, amewataka wananchi na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya taka hatarishi nchini kuzingatia matakwa ya Kanuni Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Taka Hatarishi za Mwaka, 2021 ikiwemo kuwa na kibali kilichotolewa na Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.
Sanjari na hilo, Waziri Jafo ametoa tahadhari kwa yeyote anayejishughulisha na shughuli za kukusanya, kuhifadhi, kusafirisha ndani ya nchi, kuingiza nchini, kusafirisha nje ya nchi na kupitisha nchini taka hatarishi bila kibali, atakuwa ametenda kosa la kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 na Kanuni zake, Ofisi ya Makamu wa Rais imepewa Mamlaka ya kusimamia na kuratibu masuala yote yanayohusu Mazingira nchini. Kifungu cha 133(1) na (3) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 pamoja na Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka Hatarishi za Mwaka 2021, zinampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Mazingira kutoa vibali vya kukusanya, kuhifadhi, kusafirisha ndani ya nchi, kuingiza nchini, kusafirisha nje ya nchi na kupitisha nchini taka hatarishi.
Aidha, taka hatarishi au taka zenye madhara ni pamoja na vyuma chakavu, taka za kieletroniki, dutu hatarishi, mafuta machafu, matairi chakavu, taka za plastiki, taka zitokanazo na huduma za kitabibu, betri zilizotumika na aina ya taka zote zinazotoka migodini.
Taka hizi hatarishi zinaweza kusabisha athari kwa afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira. Ili kuzuia na kudhibiti athari hizo zitokanazo na taka zenye madhara, mfumo mahsusi unaofanya kazi kwa ufanisi wa kudhibiti taka hizi unapaswa ufuatwe kama ulivyobainishwa kwenye Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 na Kanuni zake.