Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema taasisi zilizoanza kutumia nishati safi hususan gesi ambayo ni gharama ndogo, zimefanikiwa kuokoa fedha ambazo zingetumika kununulia mkaa au kuni.
Pia amesema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi zake ili zifikie lengo la kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa. Amesema hayo wakati wa mahojiano na Kituo cha Uhuru FM jijini Dodoma leo Februari 21, 2024 kuhusu utekelezaji wa katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi huku akisisitiza katazo hilo haliwahusu wananchi ngazi ya kaya.
Dkt. Jafo amesema kuwa sekta ya elimu kupitia taasisi zake zikiwemo shule ambazo zimetekeleza agizo hilo kwa asilimia 85, zimesaidia kuokoa fedha na miti ambayo ingekatwa kwa ajili ya nishati ya kupikia.
“Unakumbuka kila mwaka wa bajeti huwa tunatenga fedha kwa ajili ya matumizi mengineyo ambayo huwa yanaenda kwenye matumizi ya kuni na mkaa, sasa inaonyesha wazi waliongia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia wameweza kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha za serikali, nitoe mfano Shule ya Sekondari ya Ruvu ambayo mwanzo walikuwa wanatumia wastanii wa shilingi milioni 6 kwa mwezi lakini tangu wahamie kwenye nishati safi ya kupikia wanatumia shilingi milioni 2 kwa mwezi, sasa utaona kwa mwaka wanaokoa shilingi ngapi,”
“Hiyo ni kwa upande wa kipato, eneo la pili ni upande wa afya, tunafahamu matumizi ya kuni na mkaa yana madhara makubwa ya kiafya hasa suala zima la magonjwa ya mfumo ya upumuaji na faida nyingine ni kwenye utunzaji wa mazingira, takwimu zinaonyesha Tanzania zaidi ya hekta laki 462 kila mwaka zinapotea kwa ajili ya kuni na mkaa maana yake hii idadi ya watu wanaoenda kuacha matumizi ya kuni na mkaa itasababisha kuokoa misitu yetu,”amesema.
Pamoja na hayo pia Dkt. Jafo amesema kuwa ukame huathiri kilimo kwa kuwa asilimia kubwa ya sekta hiyo hiyo hutegemea mvua, hivyo wananchi wanahimizwa kupanda miti badala ya kuikata.
Hata hivyo, amesema Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere unahitaji mvua za kutosha, hivyo wananchi wana kila sababu ya kushiriki kikamilifu katika kutunza misitu iliyopo ili tupate mvua za kutosha.
Kwa upande mwingine amewapongeza mabalozi wa mazingira kwa kujitoa kwao katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya utunzaji wa mazingira kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Amesema hamasa hiyo ni chachu kwa kampeni mbalimbali za hifadhi ya mazingira hususan ile ya Soma na Mti inayowahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo nchini ambao hutakiwa kupanda miti na kuitunza.