Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo –Mwanza
Wizara zote zinazohusika na Vyama vya Ushirika kwa Akiba na Mikopo (SCCULT) zimetakiwa kuhakikisha kwamba zinakuwa na dawati la Ushirika na taarifa zake kuwasilishwa kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania.
Pia, Tume ya Maendeleo ya Ushirika imetakiwa kuhakikisha kuwa inasimamia, kudhibiti na kuhamasisha Vyama vya Ushirika viweze kufanya kazi kikamilifu na kwa wakati kwa kuzingatia Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015; na kanuni za Vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo ya 2014.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye kongamano la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika linalofanyika mkoani mwanza katika ukumbi wa Malaika Beach Resort leo tarehe 27 Machi 2019.
Mhe Hasunga alisema kuwa mamlaka zote zinazohusika na Maendeleo ya Sekta ya Ushirika nchini zijiwekee malengo yanayotekelezeka ya kusukuma gurudumu la Maendeleo ya ushirika na kujipima kila mara.
Kadhalika Serikali imesema kuwa itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wote wanaobainika kuhujumu dhamira njema ya maendeleo ya ushirika kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na matarajio ya kuanzishwa kwa vyama hivyo.
Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Ushirika inakua na kujisimamia vema katika utekelezaji wa majukumu yake japo bado kuna wabadhilifu wachache wanaoendelea kubainika.
Alisema kuwa Ushirika wa Akiba na Mikopo una umuhimu mkubwa katika jamii kwani unajenga Jamii yenye utamaduni wa kuweka akiba ya fedha mara kwa mara na kuwa namatumizi bora ya fedha zao kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya siku za usoni, Kuanzishwa kwa SACCOS nyingi katika maeneo mengi ya vijijini, ambazo zimesogeza karibu huduma za kifedha kwa wananchi wa kawaida, Kuwawezesha kumiliki na kuendesha taasisi yao wenyewe ya fedha; na Kutoa mikopo kwa wanachama wake kwa masharti na riba nafuu wanayojiwekea wao wenyewe kwa mujibu wa Sheria na Kanuni kwa ajili ya Kuboresha maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.
Vilevile umuhimu wake ni pamoja na kushiriki katika mipango ya Serikali ikiwemo kuanzisha ajira na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, kwa kuajiri watendaji katika ngazi mbalimbali kwenye SACCOS zenyewe na kwenye miradi inayoanzishwa na wanachama wa SACCOS, Kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa wananchi wa kawaida na kuimarisha nidhamu ya fedha, Kuwajengea Wanachama hali ya kujitegemea wao wenyewe kwa kuwawezesha kukopa katika Chama chao badala ya kukopa kwa watubinafsi au benki za biashara ambazo hutoa masharti magumu na Kuwawezesha Wanachama kupata huduma za Bima katika shughuli zao.
Alisema SCCULT imejiendesha kwa udhaifu kwa kutotoa huduma stahiki kwa wanachama wake kwa muda mrefu takribani Miaka 10, kipindi hicho ikiwa na idadi ya Wanachama 1,247. hadi kufikia mwaka 2019 Januari zoezi la uhakiki juu ya uwepo wa wanachama hawa kama wapo hai na wanafanya shughuli zao umebaini takribani Vyama wanachama 500 tu ambavyo vipo hai na vinafanya kazi.