Wazee nchini wamehamasishwa kujiunga na Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) kwa kuwa elimu hiyo ina mchango mkubwa kwenye kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa na mmoja wa wanafunzi chini ya mpango huo, Bi. Masha Sogoma (65) wakati wa Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yanayofanyika Kitaifa wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo amesema tangu kujiunga na Mpango huo amenufaika na elimu ya darasani na ujasiriamali ambapo kwa sasa anajishughulisha na shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato ikiwemo utengenezaji wa bidhaa za batiki, sabuni, dawa za kuchua, mafuta ya kupika pamoja na sabuni za mlonge.
“Ninawashauri wazee ambao hawajapata hii elimu waingie ili iwasaidie. Nimeamua kwenda shule na baada ya kusoma tukawezeshwa tujifunze ujasiriamali ili tusikae tu bila kuwa na kitu cha kutuingizia kipato, naiomba Serikali kuweka mkakati wa kuwafikia wazee wengi zaidi vijijini ambao hawajafikiwa na elimu hiyo,” amesema.
Naye Mwalimu wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) pamoja na Kisomo chenye Manufaa na Mwendelezo (KCM), Bi. Rehema Gabriel amesema ana darasa la wazee kuanzia miaka 60 na kuendelea anaowafundisha katika kituo cha wazee kilichopo Shule ya Msingi Mwendapole ‘A’ mkoani Pwani na darasa lingine la Kisomo chenye manufaa na mwendelezo linapatikana eneo la CCM Wilaya ya Kibaha.
Kwa mujibu wa Mwl. Rehema wanafunzi wake hao wanaingia darasani kujifunza KKK na stadi za kazi, kisha kupata mafunzo ya Ujasiriamali. Amesema wanafunzi hao wazee wanajifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo mafuta, sabuni, batiki, mkaa, lishe, sabuni za usafi na bidhaa nyinginezo nyingi ambapo darasa lake la wazee lililopo eneo la Shule ya Msingi Mwendapole A lina wanafunzi 72 na limegawanyika katika madarasa mawili.
“Katika darasa hilo unawabembeleza wazee kama wanafunzi wa chekechea ili waingie darasani, na lile darasa lingine ni la wanafunzi waliosoma zamani ambao sasa tunawakumbushia, lengo la elimu ya wazee ni kutoa dhana iliyojengeka katika jamii kuwa mtu akishakuwa mzee hana maana,” amesema.
“Uzee sio kuishia bali ni hazina hivyo tunachota hazina za wazee, kule ziliko na kuzileta huku,” alisema na kuongeza kuwa darasa lake lingine lina wazee 30.
Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo kwa Walimu wa madarasa hayo ya wazee ili kuongeza uzoefu wa kufundisha, kwa kuwa mzee ni kama mtoto anahitaji kubembelezwa.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Profesa Michael Ng’umbi amesema wajibu wao ni kuhamasisha jamii kuona elimu ya watu wazima bado ni nyenzo muhimu katika kujenga utu, kuhakikisha kwamba haki ya msingi ya binadamu ya kujua kusoma, kuandika na kuendelea kujifunza muda wote inazingatiwa.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Taaluma, utafiti na ushauri, Dkt. Philipo Sanga amesema umuhimu wa elimu hiyo ya watu wazima ni kumuandaa mtu katika maendeleo endelevu.
“Elimu ya watoto tunasema inaandaa watoto kwa ajili ya maisha ya baadaye lakini wanapojifunza watu wazima ni kwa ajili ya kujifunza sasa,” amesema.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ipo katika maadhimisho ya juma la Elimu ya Watu Wazima kitaifa Kibaha maili moja mkoani Pwani