Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wazabuni 66 wajitokeza mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge.
Sep 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_14452" align="aligncenter" width="750"] Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha Umeme wa Megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani, Mhandisi Leonard Masanja, (katikati) akisikiliza jambo kutoka kwa Wazabuni walionunua nyaraka za ujenzi wa mradi huo. kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya manunuzi wa Wizara ya Nishati na Madini, Amon macAchayo.[/caption]

Na Zuena Msuya - Dar es Salaam.

Takribani wazabuni 66 kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kununua Nyaraka za Zabuni  za ujenzi wa mradi wa Umeme wa kiasi cha megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) mkoani Pwani hadi kufikia tarehe 19 Septemba, 2017.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia ujenzi wa mradi huo, Mhandisi Leonard Masanja wakati wa mkutano na wazabuni hao uliofanyika Jijini Dar es salaam, Septemba 18, 2017. Mkutano huo ulilenga kutoa maelezo mbalimbali kuhusu mradi kwa wazabuni hao.

Hata hivyo, Mhandisi Masanja aliweka wazi kuwa, Serikali bado inaendelea na zoezi la kuuza nyaraka za zabuni hizo, ambapo tarehe ya mwisho ya kuzirudisha kwa ajili ya kuzifanyia tathmini na  kumpata mshindi wa zabuni hiyo ni Oktoba 16, 2017.

[caption id="attachment_14454" align="aligncenter" width="750"] Wazabuni (Kampuni na Wakandarasi) mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi walionunua Nyaraka za Zabuni( Tender Document) za Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mradi huo( hayupo pichani).[/caption]

Akieleza kuhusu mkutano na wazabuni hao ambao ni makampuni na wakandarasi mbalimbali, Mhandisi Masanja alisema kuwa, wazabuni hao walipatiwa maelezo hayo baada ya kutembelea eneo la mradi na kujionea hali halisi ya eneo husika.

Aidha alisema kuwa, katika mkutano huo, wazabuni hao walipata fursa ya kuuliza maswali na kueleza changamoto mbalimbali walizoona kwenye eneo la mradi na katika nyaraka za zabuni ambapo baadhi ya maswali yao yalijibiwa papo hapo na mengine kuandaliwa na kusambazwa kwa wazabuni wote walionunua nyaraka za zabuni.

Agosti 30, 2017, Serikali kupitia Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani ilitangaza zabuni ya kuanza ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Umeme wa megawati 2100 katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Stiegler’s Gorge)

Dkt. Kalemani  alifafanua kuwa tayari taratibu za awali zilikwishaanza ambapo wataalam  wa ndani na nje walishakutana na kuchagua sehemu za kujenga mradi huo katika Mto Rufiji, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) lilishaanza upembuzi yakinifu wa kujenga miundombinu ya kufikisha huduma umeme katika eneo la mradi utakotumika wakati wa ujenzi na Wakala wa Barabara nchini  (TANROADS) kujenga miundombinu ya  Barabara.

Sambamba na hilo, Dkt. Kalemani aliweka wazi kuwa mkandarasi atakayepewa kazi ya kujenga mradi huo ni yule tu atakayeridhia kujenga mradi kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi ndani ya kipindi cha miezi 36.

Alisema kuwa tayari Serikali imetenga fedha za kutekeleza mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baada ya kumpata mzabuni na  kuanza ujenzi wake.

Mradi huo utakapokamilika utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Umeme nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi