Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amewaomba Wamiliki wa Shule zisizo za Serikali nchini kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya mafunzo ya amali ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inatarajia kuyatilia mkazo kama mapendekezo ya Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 na mabadiliko ya Mtaala wa Elimu ya Awali, Msingi , Sekondari na Ualimu yatapitishwa na Mamlaka husika.
Waziri Mkenda ameyasema hayo Oktoba 10, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano kati ya Wizara hiyo na Wamiliki wa Shule mbalimbali nchini.
Amesema kuwa, Serikali itajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuona ni kwa jinsi gani watasaidia Sekta Binafsi ambao watapenda kuwekeza katika mkondo wa mafunzo ya amali kwani Serikali pekee haitoweza kuanza kwa kasi kwa sababu lazima kuwe na uwekezaji wa kutosha kwani ni dhahiri kuwa watu wataunyanyapaa mkondo wa mafunzo ya amali kama utaanzishwa bila kuwekeza vya kutosha.
“Kuna baadhi ya Shule za Mafunzo ya Amali zipo, zingine tutazifufua, lakini tutaziongezea zaidi. Tunapenda kuwahamasisha wawekezaji wanaohitaji kuwekeza kwenye sekta binafsi wawekeze kwenye upande wa mafunzo ya amali, nawaomba tushikane mikono kwa pamoja kwani tunawahitaji sana kuwekeza katika mkondo huu.” Amesema Prof. Mkenda.
Vile vile, amewashukuru Wamiliki wa shule mbalimbali nchini pamoja na wadau wa elimu kwa kuwekeza katika ujenzi bora wa shule ambapo wameongeza fursa kwa wazazi kuchagua ni wapi wawapeleke watoto wao kupata elimu bora hapa hapa nchini kwani zamani wengi wao walikuwa wakisafiri hadi nje ya nchi kutafuta shule zilizo bora.
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan kati ya vitu ambavyo vinamtambulisha ni kuweka msukumo mkubwa na wepesi wa kufanya biashara na kukuza uwekezaji ivyo, katika kutekeleza maelekezo ya Rais wetu tumeona tuwasikilize ili tufahamu ni nni tunatakiwa kukifanya kuleta wepesi katika uwekezaji na uendeshaji wa shule zetu, nyie sio maadui wala changamoto bali ninyi ni fursa na msaada mkubwa kwa Serikali katika kuimarisha elimu.”
Akifafanua kuhusu kuanza kutumika kwa mitaala mipya ya elimu, Waziri Mkenda amesema, mitaala hiyo inatarajiwa kuanza Januari, 2024 kwani vitabu vya ziada na kiada vilivyopo bado ni muhimu na vitatumika, kikubwa ni kuandaa Walimu ambao nao mabadiliko ya utoaji mafunzo sio makubwa.
Amemalizia kwa kufafanua kuwa kama mapendekezo yatakayojadiliwa katika kikao hicho yatapita kama yalivyokuwa, mitaala mipya itaanza kutumika kwa wanaoanza Shule ya Msingi mpaka waliopo darasa la tatu ambao watakamilisha elimu ya msingi darasa la sita lakini itakuwa ni lazima kuendelea na shule mpaka kidato cha nne, wengine watakaoanza na mitaala hiyo ni Kidato cha Kwanza, Kidato cha Tano na Elimu ya Ualimu mwaka wa kwanza.