[caption id="attachment_40515" align="aligncenter" width="1000"] Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akihutubia Madiwani na watendaji wa mitaa na kata wa Manispaa ya Songea leo kuhusu udhibiti wa mapato ya ndani ya serikali.[/caption]
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi watatu wa idara ya fedha wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mndeme ametoa agizo hilo leo Ijumaa wakati akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani maalum kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mwaka 2019/2020 ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Amemtaja mtumishi Mhasibu (Cashier), Juliana Rocky Likunguwala kwa kosa la kusababisha hasara ya shilingi milioni mia moja na kumi na nane ambazo imebainika alizichukua kwa njia ya kutoa risiti bandia za wateja.
Mkuu huyo wa mkoa amesema mhasibu huyo kwa kipindi cha miezi mitano tangu Julai 2018 hadi Novemba 2018 ameibia Manispaa ya Songea kiasi cha shilingi milioni 118 za Manispaa ya Songea.
“Mtumishi huyu Juliana Rocky anatuhumiwa kutoa risiti bandia kwa wateja wanaoleta fedha za makusanyo ya mapato ya ndani ili ziingizwe kwenye mfumo wa malipo ya serikali” amesema mkuu wa mkoa.
Mndeme amesema uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa mhasibu huyo alishindwa kupeleka fedha benki kwa mujibu wa utaratibu
[caption id="attachment_40517" align="aligncenter" width="1000"] Sehemu ya Madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakifuatilia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma alipowahutubia leo .Lengo la kikoa hicho ni kuelezea umuhimu wa kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani ya serikali.[/caption]“Fedha hizi zilizoibwa zingeweza kujenga zahanati na hata madarasa kusaidia maendeleo ya wananchi, lakini zimeibwa na mtumishi wa umma” Mndeme amesema Serikali haitosita kuchukua hatua kali kwa watumishi wanaojihusisha na ubadhirifu.
Aidha anatuhumiwa kwa kosa la kuchukua fedha za serikali na kutumia kwenye masuala binasfi kinyume na taratibu na sheria za fedha za umma
Kufuatia agizo hilo, Mkuu wa Mkoa alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma SACP Gemin Mushy kumtafuta na kumkamata mhasibu huyo mara moja na kumpeleka mahabusu.
“RPC mtafute Juliana popote alipo na umweke ndani masaa 48 akisubiri utaratibu wa kisheria wa kumfikisha mahakamani kutokana na ubadhirifu wa fedha za umma” aliagiza Mndeme.
Wakati huo huo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma ameagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo kuwasimamisha kazi watumishi wawili wa Idara ya Fedha.
Amewata watumishi hao kuwa ni Mtunza Hazina wa Manispaa ya Songea, Denis Mwaitete kwa kosa la kushindwa kusimamamia idara ya fedha hata kupelekea ubadhirifu wa fedha Tsh 118 milioni
Mtumishi mwingine aliyetajwa kusimamishwa kazi ni Mhasibu wa Mapato wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Salum Mwaru kwa kosa la kushindwa kusimamia vema makusanyo ya fedha za mapato ya ndani.
Mkuu wa Mkoa Mndeme ametoa uamuzi wa kuwasimamisha kazi watumishi hao kufuatia uchunguzi uliofanywa na timu ya mkoa kuhusu mwenendo wa ukusanyaji mapato ya ndani katika Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma kutofanya vizuri mwaka 2018/2019