Na Beatrice Lyimo - MAELEZO, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewaasa watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu kwa maendeleo ya taifa.
Dkt. Chaula ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku nane ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) iliyoboreshwa leo mjini Dodoma.
“Nina imani kila mtu kwa nafasi aliyonayo anatakiwa kutimiza wajibu wake kufanya kazi kwa weledi na uwajibikaji kulingana na ujuzi alionao” ameseza Dkt. Chaula.
Aidha Dkt. Chaula ametoa wito kwa watumishi wa Serikali kuwajibika kwa kufuata Sera ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Chama kilichopo madarakani ambacho kina mkataba na wananchi wa kuwatumikia.
“Watendaji wa Serikali hawapaswi kuwa na Chama, wanapaswa kufuata ilani ya Chama tawala kilichopo madarakani na utekelezaji wake ni mkataba kati ya Chama na Wananchi” amesema Dkt. Chaula.
Hata hivyo, Dkt. Chaula ameupongeza Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) kwa mafunzo hayo kwani Mfumo wa kielektroniki wa kuandaa Mipango, Bajeti na Ripoti za Mamlaka ya Serikali za Mitaa (PlanRep) umekuwa mkombozi wa changamoto zilizokuwa awali katika uaandaaji wa Mipango na Bajeti za Serikali.
Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Mifumo ya TEHAMA kutoka Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) Desderi Wengaa ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ushirikiano katika kufanikisha mradi.
“Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) umejipanga katika kuzisaidia Halmashauri zote nchi nzima ambapo timu za wawezeshaji zitakwenda kila Halmashauri kuona utekelezaji wa mafunzo kwa wale ambao wamepata mafunzo haya” alisema Bw. Wengaa.
Aidha, Bw. Wengaa ameongeza kuwa katika kipindi cha uandaaji wa bajeti za Serikali yaani mwezi Octoba timu za wawezeshaji zitakwenda kila Halmashauri kwa miongozo mbalimbali ya mfumo huo.
Naye mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo Bw. Bartholome Temba kwa niaba ya washiriki wenzake ameushukuru uongozi wa Mradi wa Uimarishaji Sekta za Umma (PS3) kwa mafunzo waliopatiwa na kuahidi kutekeleza vyema mfumo huo kwa maendeleo ya Taifa.