Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Arusha
Serikali itaendelea kushirikiana na wasanii nchini ili kuhakikisha sekta ya sanaa inasonga mbele na kuwanufaisha wasanii na taifa kwa kazi wanazozifanya ikizingatiwa waasanii ni kioo cha jamii.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amesema hayo kwa niaba ya Serikali alipokuwa jijini Arusha wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Chama cha Muziki Tanzania (TaMuFo) Dkt. Donald Kisanga katika viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha jijini humo ambaye aliyefariki Agosti 9, 2020 jijini Dodoma kwa ajali ya gari.
Naibu Waziri Shonza amebainisha kuwa miongoni mwa kazi alizofanya Dkt. Donald Kisanga ni kuhakikisha wasani wa muziki wa injili wananufaika na kazi zao ambayo tayari Serikali imelifanyia kazi.
“Namshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusikia kilio cha wasanii nchini kwa kuihamishia COSOTA taasisi inasimamia haki za wasanii Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Sekta ya Sanaa nchini. Kwa hiyo naamini zile haki za wasanii ambazo walikuwa hawanufaiki na matunda ya kazi zao, sasa naamini mwarobaini umepatikana kama alivyokuwa akiamini Dkt. Donald Kisanga” alisema Naibu Waziri Shonza.
Wakati wa uhai wake Dkt. Kisanga amekuwa sio mtu wa kukata tamaa, hakusita kwenda Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) amefanikisha wasanii wengi kuwa na Bima ya afya hatua ambayo ilitokana na ushirikiano wake na Serikali na vyombo vingine ambavyo vipo chini yake ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuhakikisha wasanii wa muziki wanapata Bima ya Afya ambayo imekuwa na manufaa kwao.
Aidha, amewataka wasanii nchini waendeleze umoja kati yao wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ikizingatiwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu huku wakitanguliza mbele maslahi ya taifa.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kalvary, Dastan Maboya alisema Dkt. Donald Kisanga alikuwa anawaza juu ya taifa lake na alikuwa ni mtu ambaye haangalii dini ya mtu bali alikuwa akisimamia maono ambayo Mungu alimpa ili kusaidia taifa.