Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Watakiwa Kutembelea Ofisi za TRA Kuwasilisha Maoni na Kero za Kikodi
May 30, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_43740" align="aligncenter" width="800"]
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.[/caption]

Peter Haule, WFM, Dodoma

Serikali imetoa wito kwa wananchi kutembelea ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizopo katika maeneo yao na kuhudhuria vikao vinavyoitishwa na wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kuwasilisha maoni na kero zao zinazohusu kodi.

Wito huo umetolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Jaku Hashimu Ayoub, alietaka kujua ni lini TRA itakaa na Wafanyabiashara kusikiliza vilio vyao kwa kuwa kila mkoa una ofisi za Mamlaka hiyo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, TRA ina ofisi katika mikoa yote ya Tanzania pamoja na baadhi ya wilaya zake, na baadhi ya mikoa ina vituo maalum vya huduma za kodi (Tax Centres), hususani Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya, pia kila Mkoa una Mwanasheria na Afisa Elimu ya Kodi  kwa ajili ya kutoa elimu, kusikiliza na kutatua kero za walipakodi.

“TRA imeweka utaratibu kwa meneja wa mikoa ya kikodi kukutana na walipakodi kila Alhamisi ili kusikiliza kero zao na kuzitatua, hatua ambayo ina lengo la kujenga imani , kutatua kero na kukuza ridhaa ya ulipaji kodi kwa hiari”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa miongoni mwa kazi za kila siku za TRA ni kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara ili kuwawezesha kufanya biashara zao bila usumbufu, hivyo hufanya biashara katika ngazi ya wilaya, mikoa na Taifa ili kutoa elimu, na pia hurusha vipindi maalum katika runinga na redio kuhusu elimu ya kodi kwa wananchi na kujibu kero za wafanyabiashara.

Dkt. Kijaji alieleza kuwa Wenyeviti wa Kamati za Mapato za Mikoa na Wilaya ambao ni wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakisikiliza kero za walipa kodi kwa kushirikiana na TRA na kwamba Mamlaka hiyo hubuni na kuanzisha mifumo, vituo na vilabu rafiki vya kikodi ili kujibu vilio vya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Aidha Dkt. Kijaji alikanusha kuwepo kwa usumbufu wa utoaji wa mizigo kutoka Zanzibar ikilinganishwa na mizigo mingine inayopitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi za nje kama Zambia, Uganda, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo akifafanua kuwa bidhaa zote zinatakiwa kufuata utaratibu wa forodha.

Alisema bidhaa zinazoingia Tanzania Bara kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC), hupata msamaha wa ushuru wa Forodha lakini hulipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani pamoja na ushuru wa bidhaa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi