Wananchi wametakiwa kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, hususan vipimo vya saratani, ili kubaini ugonjwa huo katika hatua za awali na kuongeza uwezekano wa kupata matibabu na kupona.
Wito huo umetolewa Agosti 19, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na mwelekeo wa utekelezaji wa miradi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAEALEZO jijini Dodoma.

Dkt. Msemo amesema kuwa ugonjwa huo unatibika endapo utagundulika mapema na mgonjwa kupata matibabu kwa wakati huku akitaja changamoto kubwa ni pale wagonjwa wanapofika katika vituo vya matibabu wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa, hali inayoweza kupunguza uwezekano wa kupona, badala yake hupewa matibabu ya kupunguza makali ya ugonjwa pamoja na kuboresha maisha yao.
“Saratani inatibika nawaomba wananchi kutosambaza taarifa zisizo sahihi zinazoweza kuwafanya watu kuogopa kupima au kutafuta matibabu na nawaomba waandishi wa habari kutumia nafasi yanu kuelimisha na kuhamasisha wananchi kupima afya zao, kwani ugonjwa huu unapogundulika mapema, mgonjwa hupata nafasi kubwa ya kuendelea na shughuli zake za kawaida", amesema Dkt. Msemo.

Aidha, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uchunguzi, amesema kuwa Taasisi yake imekuwa ikitekeleza mpango wa huduma za mkoba unaohusisha timu za wataalamu kwenda maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa saratani.
Ameongeza kuwa kupitia mpango huo, wamefika katika maeneo mbalimbali nchini na kufanya uchunguzi kwa wananchi takribani 200,000. Baadhi yao waliobainika kuwa na saratani katika hatua za awali wameweza kupata matibabu mapema, huku wale waliobainika katika hatua za juu wakiendelea kupata matibabu ya kupunguza makali ya ugonjwa na mateso yanayotokana na saratani.

Sambamba na hilo, Dkt. Msemo amesema kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha huduma za kupambana na ugonjwa wa Saratani zinasogezwa karibu na wananchi. Ambapo ORCI ina mpango wa kupanua huduma kwa kuanzisha vituo vya saratani katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Arusha, Kigoma na Mtwara. Aidha, kwa Arusha Taasisi hiyo tayari imepata eneo lenye ukubwa wa ekari 18 kwa ajili ya kuendeleza mradi huo.