Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

VETA: Fursa za Uchumi Zipo, Kinachohitajika ni Ujuzi
Sep 04, 2026
VETA: Fursa za Uchumi Zipo, Kinachohitajika ni Ujuzi
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Na Bupe Mwaiseje - MAELEZO

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, amesema ukuaji wa uchumi, uwekezaji na sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, ujenzi, madini, kilimo cha kisasa, nishati, utalii na teknolojia umeongeza mahitaji ya Watanzania wenye ujuzi wa kiufundi.

Amesema VETA imejipanga kuhakikisha vijana wanapata stadi zinazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine, ili kutumia fursa zinazozalishwa na ukuaji wa uchumi.

Akizungumza  katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26, Septemba 4, 2026,  CPA. Kasore amesema fursa za ajira zinaendelea kuongezeka katika sekta mbalimbali, lakini changamoto ni upatikanaji wa watu wenye ujuzi unaohitajika.

“Kwa hiyo fursa zipo, kinachohitajika ni ujuzi. Tunapomwambia kijana ajifunze ufundi stadi, tunamwambia ajifunze kwa sababu uchumi unaendelea kumhitaji,” amesema.

Amesema VETA imeongeza udahili kutoka wanachuo 69,347 mwaka 2022/23 hadi 116,468 mwaka 2025/26, huku Serikali ikiendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vipya 65 vinavyotarajiwa kuanza kutoa mafunzo Januari 2027.

Aidha, amesema katika kipindi cha 2023/24 hadi 2025/26, jumla ya wahitimu 117,953 walitunukiwa vyeti vya ufundi stadi, huku mafundi 18,008 wakirasimishiwa ujuzi wao kupitia Programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi (RPL).

VETA pia imeendelea kuoanisha mafunzo na mahitaji ya uchumi kwa kuboresha mitaala, kuimarisha mafunzo mahali pa kazi na ushirikiano na waajiri na viwanda, pamoja na kuwekeza katika vifaa vya kisasa. Mwaka 2024/25, vifaa vyenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 9.596 vilinunuliwa, huku bunifu 17 zikifikia hatua mbalimbali za ubiasharishaji.

Katika sekta ya madini, kupitia Programu ya Mafunzo ya Ufundi kwa Shughuli za Uchimbaji Madini (IMTT), vijana zaidi ya 1,688 wamenufaika na mafunzo, huku mitaala sita mipya ya uchimbaji madini chini ya ardhi ikiandaliwa.

Kwa upande wa Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye Tija Awamu ya Pili ( ESPJ II), amesema VETA inalenga kuimarisha vituo 15 vya umahiri, kurasimisha ujuzi wa mafundi 84,000 na kuwafikia wakufunzi na wanafunzi 100,000 kupitia jukwaa la kitaifa la mafunzo ya ufundi stadi kidijitali.

CPA. Kasore amesema VETA inalenga kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi itakayochochea uchumi, teknolojia na uzalishaji.

“Tusimwambie mtoto wetu, ‘ukifeli shule utasoma ufundi.’ Tumwambie, ‘ukitaka kuwa na ujuzi wa kujenga maisha na kujenga Taifa, soma ufundi stadi,’” amesisitiza.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor