Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umerahisisha upatikanaji wa zabuni kwa wazawa na makundi maalum katika zabuni za Serikali, huku vikundi maalum 27, 946 vikisajiliwa na kupata zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 56.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denis Simba, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Agosti 20, 2026, kuhusu utekelezaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka utaratibu wa kuhakikisha wazawa wanapata fursa katika zabuni za Serikali, ikiwemo zabuni zote zenye thamani isiyozidi Sh bilioni 50 kutengwa kwa wazabuni wazawa pekee.
“Upendeleo huu si kwa maneno tu, bali kupitia Mfumo wa NeST ni rahisi kufuatilia na kutekeleza, wazabuni wa nje hawawezi kuomba zabuni zenye thamani ya chini ya Sh bilioni 50 kwa kuwa zimewekwa kwa ajili ya wazabuni wazawa pekee,” amesema Simba
Aidha, Sheria hiyo pia imetoa upendeleo wa hadi asilimia 10 kwa wazabuni wa ndani katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa, huku bidhaa zinazozalishwa nchini zikipata upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa kutoka nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma imezielekeza taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, ambayo ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Aidha, hadi sasa jumla ya makundi maalum 27,946 yamesajiliwa katika Mfumo wa NeST, katika makundi hayo, vijana ni 13,317, wanawake 13,400, wazee 643 na watu wenye ulemavu 586.
Pamoja na hayo, Bw. Simba amesema kuwa PPRA inalenga, kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kufikisha idadi ya makundi maalum yaliyo tayari kushiriki katika zabuni hadi takribani 300,000. Ili kuongeza fursa za ajira na kazi kwa Watanzania ambao hawana uwezo wa kuanzisha kampuni, lakini wanaweza kujiunga katika vikundi na kutekeleza zabuni za Serikali.

Pia, amesema kuwa kutokana na dhamira ya Serikali ya kuwawezesha Watanzania kiuchumi, kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh milioni 500.