Kutokana na uwekezaji mkubwa unaoambatana na huduma za kisasa katika matibabu ya saratani nchini, Tanzania imechukua nafasi ya pili kwa nchi zinazopatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara katika mapambano dhidi ya magonjwa ya saratani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amebainisha hilo wakati akizungumza na Watanzania kupitia waandishi wa habari, Agosti 19, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma.

Taasisi imeshapata mafanikio makubwa kwenye utoaji wa huduma za uchunguzi wa saratani katika hatua za awali kwenye matiti, shingo ya kizazi na tezi dume.
"Serikali imenunua mashine 'Pet Scan', kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 20, ni kipimo chenye uwezo wa kugundua saratani katika hatua za awali kabisa, lengo ni kuhakikisha wagonjwa wanatibiwa kwa uhakika na kwa wakati bila kupoteza muda" - Dkt. Msemo
Vile vile amesema kuwa "Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika awamu hii ya uongozi wake amefanya mageuzi makubwa sana katika huduma za saratani, hii haijawahi kutokea katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, hii imepelekea kupata utambuzi wa kimataifa katika upambanaji wa saratani kutokana na uwekezaji alioufanya katika upanuzi wa huduma za matibabu ya saratani nchini"
Akitaja mafanikio mengine, Dkt. amesema kimejengwa kituo cha saratani Mbeya ambacho kitakamilika ifikapo Desemba 2026, na Juni 2027 kitakuwa katika hali nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi huku akitaja gharama zake kuwa Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 11 katika ujenzi pekee, huku ikikadiriwa kutumia takribani Shilingi bilioni 10 katika vifaa tiba.

"Lengo la uwekezaji huu ni kuwahudumia wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na nchi za jirani ikiwemo Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hii pia itasaidia kustawisha tiba utalii" amejuza Dkt. Msemo
Akitaja sababu kuu ya Serikali kujenga vituo vya huduma maalum za kitabibu sehemu mbalimbali za nchi, amesema ni pamoja na kuondoa gharama na usumbufu wa wananchi kusafiri mwendo mrefu kufuata huduma mbali, mathalani mtu kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam kutibiwa saratani.
"Hata katika majengo ya taasisi yetu Dar es Salaam, Serikali inaendelea na uwekezaji mkubwa wa jengo la kisasa litakalokuwa na maabara ya kisasa ya tiba kemikali, sehemu za kliniki za kuwaona wagonjwa, wodi za wagonjwa na duka la dawa, ofisi za watumishi" - Dkt. Msemo
Akizidi kufafanua baadhi ya vifaa tiba vilivyopo katika taasisi yake, amesema, wanashukuru sana, kwa sasa, pamoja na mashine zingine nyingi za mionzi walizonazo, lakini wamefungiwa mashine kubwa ya kutibu wagonjwa ya takribani zaidi ya Shilingi bilioni 7, inayotibu saratani kwa kutumia teknolojia ya juu na kisasa na kusema mashine hizi zinapatikana kwenye nchi za magharibi, lakini hata Tanzania katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ipo.

Dkt. amesema mafanikio ni mengi ambayo taasisi ya Saratani Ocean Road inayo kwa sasa katika kutoa matibabu kwa wagonjwa na kuwatoa wananchi wasiwasi wa kuwa na imani potofu kwamba saratani haiponi.
"Wanaamini kuwa ukipata saratani hauponi, hapana. Katika magonjwa yasiyo ya kuambukiza, saratani ni mojawapo na inatibika na unaachana na ugonjwa huo cha msingi ni kuwahi kuanza matibabu na si kusubiri ugonjwa kufika hatua mbaya" - Dkt. Diwani Msemo
Mafanikio mengine aliyoyataja ni ujenzi wa vituo vya saratani mkoani Arusha, Kigoma na Mtwara, ambapo Arusha kitajengwa pia kiwanda cha madawa ya saratani.
"Ukiamua kwenda India na kwingineko kutibwa saratani ni wewe tu umependa, ila kwetu sasa hivi yote yanapatikana, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kutoa huduma kwa wananchi kwani inatekeleza kauli ya afya ni msingi na mtaji wa maendeleo" amesema Dkt. Msemo