Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, amesema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, kutaimarisha mazingira ya utendaji wa Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Kabudi amesema hayo Septemba 6, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa majengo ya Ofisi za Wizara, Taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, ambao unalenga kuendelea kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.

Amesema ujenzi wa majengo ya Wizara na Taasisi za Serikali katika awamu ya pili unatekelezwa kwa kiasi kikubwa na wakandarasi na watoa huduma wa ndani ya nchi, ambapo jumla ya Wakandarasi 11 wanahusika, kati yao watano wakiwa taasisi za Serikali na sita kutoka Sekta Binafsi.
Ameeleza kuwa kazi hizo pia zinasimamiwa na washauri elekezi watano ambao wote ni taasisi za Serikali, zikiwemo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Ushauri ya Chuo Kikuu Ardhi (ABECC), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) pamoja na Kampuni ya Watumishi Housing Investment.
“Tasisi mbalimbali za Serikali zimehusika katika ujenzi na usimamizi wa huduma muhimu, ambapo TARURA inatekeleza ujenzi wa barabara na miundombinu yake, DUWASA inajenga mifumo ya maji safi na maji taka, huku TANESCO ikijenga miundombinu ya umeme na TTCL ikiweka mifumo ya mawasiliano” amesema Prof. Kabudi

Amesema TEMESA imehusika katika usimikaji wa mfumo wa kamera za usalama (CCTV), Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) katika kuunganisha majengo na mifumo ya TEHAMA, TPDC katika mfumo wa gesi asilia, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika ujenzi wa vituo vya huduma za zimamoto na uokoaji, huku TFS ikitekeleza upandaji miti na uendelezaji wa mandhari ya Mji wa Serikali.
Prof. Kabudi amesema ubunifu wa majengo na miundombinu iliyojengwa katika awamu ya pili umezingatia dhana ya kuwa na Mji Janja (Smart City), ikiwemo matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, dhana ya mji wa kijani, Sheria za Mipango Miji, Mpango Kabambe wa Mji wa Serikali pamoja na Tathmini ya Athari kwa Mazingira.
Amesema majengo hayo yamegawanywa katika miundo minne (Prototypes) kulingana na mahitaji ya Wizara na Taasisi, ambapo baadhi yana uwezo wa kuchukua watumishi 300, 500 na hadi 1,400, huku muundo mwingine ukiwa na uwezo wa kuchukua takribani watumishi 150.

Prof. Kabudi amesema kukamilika kwa majengo ya awamu ya pili kutawezesha jumla ya watumishi 18,510 kutumia ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuendelea kuimarisha Dodoma kama kitovu cha shughuli za Serikali.
Amesema Serikali pia imeendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa kutoa fedha za ununuzi wa samani kwa ajili ya Wizara na Taasisi 26, huku uzinduzi wa barabara za lami ukiwa sehemu ya uwekezaji unaolenga kurahisisha usafiri, mawasiliano na upatikanaji wa huduma ndani na nje ya Mji wa Serikali.