Na Jonas Kamaleki
Matumaini ya wananachi wa wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero ya kijamii na kiuchumi yarejea baada ya Daraja la Magufuli kujengwa na kuzinduliwa.
Kipindi cha zaidi ya miongo mitano ya adha, bughudha, mateso na hata watu kupoteza maisha kimeisha baada juhudi za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano kukamilisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 384 kwenye mto wa Kilombero.
Usafirishaji wa mazao kati ya wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero hadi Morogoro ilikuwa ni shida kwani njia pekee ilikuwa ni ya kutumia kivuko ambacho hakikuwa na uhakika. Suala hili liliathiri sana uchumi wa watu wa maeneo hayo na kuwafanya waishi maisha ya kimaskini huku wakiwa na mchele na mazao mengine ya kilimo yasiyo na soko.
Baada ya Rais Magufuli kuzindua daraja la mto Kilombero ambalo limepewa jina la Magufuli, wananchi wa wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutimiza ahadi waliyoitoa kwa wananchi hao ya kuwajengea daraja la mto Kilombero ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kijiji cha Kivukoni, mkoani Morogoro, wakazi hao wamesema kuwa hivi sasa changamoto zao zimetatuliwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo.“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hili kwani limekuwa mkombozi kwetu wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero kwani hapo nyuma vifo vingi vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko kufuata huduma za kijamii wilaya jirani ambapo ndio kuna huduma zote za muhimu”, amesema Bi. Zainabu Mtalanga.
Kujenga daraja ni suala moja na utunzaji wa daraja hilo ni suala jingine. Kwa mukhtadha huo, Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi, Prof. Mbarawa anatoa wito kwa wananchi hao kulilinda daraja hilo kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba kokoto chini ya daraja, kuiba alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo juu ya daraja kwani Serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja hilo na barabara unganishi katika eneo hilo.
Daraja hilo ambalo limezinduliwa na Rais Magufuli wiki iliyopita (tarehe 05 Mei, 2018) limejengwa pamoja na barabara zake zenye urefu wa kilometa 9.142 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 61.133 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kutokana na juhudi za Rais Magufuli kuboresha miundombinu nchini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemuomba Mhe. Rais Magufuli daraja hilo liitwe “Daraja la Magufuli” (Magufuli Bridge). Rais naye ameridhia daraja hilo liitwe kwa jina lake. Hii ni mara ya pili Mhe. Rais kuombwa daraja liitwe kwa jina lake na ni mara ya kwanza kukubali baada ya kukataa ombi la awali la daraja la Kigamboni ambalo Rais Magufuli alisemwa liitwe daraja la Nyerere.
Prof. Mbarawa ameamua kutoa jina hilo ikiwa ni kwa mujibu wa sheria, na amebainisha kuwa uamuzi wake huo umezingatia juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Rais Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi, ambapo baada ya kutokea ajali ya kuzama kivuko iliyosababisha takribani watu 30 kupoteza maisha mwaka 2001 alifika Ifakara, akatoa pole kwa wafiwa na akaagiza kuanza kwa mchakato wa ujenzi na kisha kuufuatilia kwa ukaribu hadi daraja hilo limekamilika.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema daraja hilo lenye njia mbili litadumu kwa miaka zaidi ya 120, lina uwezo wa kubeba tani 180 kila upande, lina njia za watembea kwa miguu na limefungwa taa zinazotumia nishati ya jua (Solar Power).
Akizungumza na wananchi wa Ifakara katika uwanja wa michezo mjini hapo Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewapongeza wananchi wa Ifakara kwa kujengewa daraja hilo, na pia amewapongeza Watanzania wote kwa kulipa kodi zilizowezesha kutekelezwa kwa mradi huo mkubwa kwa kutumia fedha zao.
Mhe. Rais Magufuli amewataka wananchi wa Ifakara, Malinyi, Kilombero, Kilosa na maeneo mengine yatakayonufaika na kujengwa kwa Daraja la Magufuli na ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara kutumia miundombinu hiyo kwa manufaa yaani kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyasafirisha kwenda kwenye masoko, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Ifakara – Malinyi – Londo hadi Lumecha Wilayani Songea ambako itaungana na barabara kuu ya Songea – Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala.
Mhe. Rais Magufuli amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kujenga uchumi na kwamba juhudi kama hizo pia zinafanyika kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia miradi ya Kinyerezi 1,2-3 na mradi wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers Gorge) itakayoiwezesha Tanzania kuwa na Megawati 5,000 za umeme ifikapo mwaka 2021, kujenga reli, kuimarisha usafiri wa anga, kulinda rasilimali ikiwemo madini na kuboresha huduma za jamii zikiwemo kutoa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuimarisha miradi ya maji na kuboresha huduma za afya.
Mhe. Rais Magufuli ambaye akiwa njiani kuelekea Ifakara alisimamishwa na wananchi wa vijiji vya Sande, Misufini, Mkula, Mang’ula, Mang’ula Kona, Kisawasawa, Kiberege na Sululu ambako alisikiliza kero zao na kuchangia fedha katika miradi ya maendeleo, aliwataka wabunge kuwajibika ipasavyo kwa kusikiliza kero za wapiga kura wao na kuzifanyia kazi badala ya kuacha kero hizo ziwasubiri viongozi wa kitaifa.
“Wabunge mna fedha za mfuko wa jimbo, wasaidieni wananchi wenu, haiwezekani wananchi wawe wanamuomba Rais fedha za kujengea matundu ya vyoo vya shule wakati nyinyi mpo” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu kero ya wananchi kuendelea kutozwa ushuru wa mazao yasiyozidi tani moja kwa mujibu wa sheria, Mhe. Rais Magufuli aliwataka viongozi kote nchini kuwashughulikia wanaotoza ushuru huo na kusisitiza kuwa “Najua viongozi wote Tanzania mnanisikia, nataka mtu atoke na mchele hapa Ifakara apeleke Dar es Salaam, apeleke Moshi, apeleke Tabora na ashuke nao mpaka Mpanda bila kubughudhiwa ilimradi hauzidi tani moja”.
Akiwa katika vijiji vya Mang’ula na Mang’ula Kona Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeanza kuchukua hatua za kukirejesha kiwanda kutengeneza vipuri cha Mang’ula ili kuhakikisha kinaendeshwa kwa malengo yaliyokusudiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Barabara na madaraja yanayowekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa ni dalili kwamba uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi kwani mazao na malighafi ya viwanda yatafikishwa viwandani kwa muda mwafaka na hatimaye bidha za viwanda zitawezakulifikia soko kwa wakati kutokana na ubora wa mioundombinu.
Usafiri wa uhakika utapunguza hata bei hivyo kuwawezesha wananchi hata wa kipato cha chini kuweza kununua bidhaa hizo. Kwa kipindi cha nyuma ilikuwa inachukua takriban siku tatu hadi nne kusafirisha mahindi toka Songea, mkoani Ruvuma na kuyafikisha Dar es Salaam, lakini baada ya kujengwa barabara za lami toka Dar es salaam hadi Songea, ni siku moja mazao hayo kusafirishwa kwa umbali ulele.
Miundombinu bora ni muhimili wa uchumi, hivyo wananchi hawanabudi kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha miundombinu. Ikumbukwe kuwa na ujenzi wa reli ya kisasa ya viwango vya kimataifa (Standard Gauge Railway) itasaidia zaidi kwenye kusafirisha tani nyingi za mazo kwa pamoja na kwa wakati muda mfupi. Takriban nchi zote duniani hutumia usafiri wa treni katika kusafirisha mizigo.
Upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme nalo ni suala muhimu sana katika ujenzi wa uchumi unaotegemea viwanda. Sanjari na ujenzi wa madaraja na barabara, ujenzi wa miundombinu ya umeme hasa mradi wa Stieglers Gorge ni ushahidi tosha kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwakomboa wananchi wake.
Mwisho.