[caption id="attachment_52630" align="aligncenter" width="750"] Afisa Mfawidhi wa THBUB Kanda ya Kusini, Bwana Noel Chiponde (kushoto) akimkaribisha Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu (katikati) katika ofisi ya Tume zilizopo mkoani Lindi alipoitembelea Mei 18,2020 . Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya.[/caption]
Na Mbaraka Kambona
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu ametoa rai kwa wananchi wanaoishi katika Mikoa ya Kusini kutoka na malalamiko na badala yake yawasilishwe katika ofisi za Tume ili yaweze kushughulikiwa.
Jaji Mwaimu aliyasema hayo Mei 18, 2020 katika ziara aliyoifanya ya kutembelea ofisi ya THBUB iliyopo mkoani Lindi ambayo inahudumia mikoa yote ya Kanda ya Kusini ikiwemo Lindi, Mtwara na Songea.
Katika ziara hiyo Jaji Mwaimu alisema kipindi cha miaka miwili iliyopita Tume haikuwa na uongozi kwa maana ya Makamishna jambo ambalo lilichangia baadhi ya kazi kusimama lakini kwa sasa Tume imekamilika hivyo wananchi waendelea kuwasilisha malalamiko yao ili waweze kusaidiwa.
[caption id="attachment_52632" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mheshimiwa Godfrey Zambi (kushoto) akimtambulisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Rehema Madenge (wa pili kushoto) kwa Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu (kulia) na ujumbe wake walipotembelea ofisi za Mkuu wa Mkoa huo Mei 18, 2020.[/caption]“Niwaeleze wananchi kwamba Tume ipo na ipo imara kuwasaidia, walete malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora na sisi tunawaahidi yatafanyiwa kazi kwa haraka”, alisema Jaji Mwaimu.
Awali akiongea na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alipomtembelea ofisini kwake alisema kuwa kimsingi tume ni taasisi iliyoundwa kuisaidia serikali kutatua kero za wananchi zinazohusiana na uvunjifu wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
“Tume ni jicho la serikali ambalo inalitumia kumulika na kubaini changamoto zinazojitokeza hususani za masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili kuiepusha serikali kuingia katika migogoro isiyo ya lazima na wananchi wake”, alieleza Jaji Mwaimu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi alimueleza Jaji Mwaimu kuwa Mkoa wa Lindi unaendelea kufunguka na kuna miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa mkoani humo hivyo sio vibaya wakaweka utaratibu wa kufuatilia miradi hiyo ili kujiridhisha kama inatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu.
Aidha, Jaji Mwaimu aliwapongeza watumishi wa THBUB wa Kanda ya Kusini kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kuhakikisha kuwa wananchi wa kanda hiyo wanapata huduma nzuri na kwa wakati.
“Kwanza mimi niwapongeze kwa kazi nzuri ambayo mmeendelea kuifanya pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo lakini mmeendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi”, aliongeza Jaji Mwaimu.
[caption id="attachment_52631" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi (katikati) akiagana na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu na ujumbe wake muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo yao Mei 18,2020. Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya.[/caption]Wananchi wa Mikoa ya Kusini wamehimizwa kutumia ofisi za Tume zilizopo katika Kanda hiyo ili iwe rahisi kwao kupata huduma, na kwa msaada zaidi THBUB imetoa anuani na mawasiliano kama ifuatavyo; S.L.P. 1050, LINDI; Simu: (023) 2202734/2202744, na kwa wale watakaotaka kuwasiliana na ofisi za Makao Makuu Dodoma wanaweza kutumia S.L.P. 1049, DODOMA; Simu: 0734 047 775/0734 119 978; Barua pepe: info@chragg.go.tz.
Jaji Mwaimu alikutana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika Mikoa ya Kusini ambayo lengo lake kubwa ni kutembelea ofisi ya Tume iliyopo mkoani Lindi ili kushughulikia malalamiko ya muda mrefu yaliyowasilishwa na wananchi katika ofisi hizo.