Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Maili Moja Wafurahia Kero ya Maji Kutatuliwa
Feb 11, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_40345" align="aligncenter" width="900"] Tanki la maji Mtaa wa Muheza, Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkoani Pwani kama linavyoonekana katika picha, mradi huo umesaidia kuondoa adha ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo na unahudumia wananchi zaidi ya 2000.[/caption]

Na: Lilian Lundo

Wananchi wa Maili Moja, mtaa wa Muheza, Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wameishukuru serikali kwa kumaliza kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.

Furaha ya wananchi hao ilionekana wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wetu mwisho wa wiki iliyopita. Wengi wa wananchi waliohojiwa wameonyesha kufurahishwa na juhudi za serikali kuwapatia wananchi wa eneo hilo huduma ya maji safi na salama na wamempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa kutatua kero ya maji iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.

"Kabla ya mradi huu kukamilika tulikuwa tukitembea umbali mrefu kutafuta maji ambapo tulikuwa tunalazimika kuamka saa nane za usiku na kurudi saa mbili asubuhi lakini kwa sasa tumesogezewa huduma ya maji karibu na makazi yetu tena kwa gharama ndogo," amesema Zawia Salum.

Filemoni Shila, mkazi wa siku nyingi eneo hilo amesema kusogezwa karibu huduma ya maji kwenye makazi yao kumesaidia kupata muda wa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato ambapo kabla ya kuwepo mradi huo  muda mwingi walikuwa wakitumia kutafuta maji.

[caption id="attachment_40346" align="aligncenter" width="1000"] Mkazi wa Mtaa wa Muheza, Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkoani Pwani Bi Zawia Salum akiteka maji katika kituo kimojawapo cha maji kilichojengwa na Serikali ya Awamu ya Tano kinachohudumia wananchi zaidi ya 2000 katika mtaa huo. Mradi huo umeigharimu Serikali Milioni 359 na kuzalisha lita 100,000 kwa siku ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.[/caption]  

Naye mwanafunzi wa Shule ya Msingi Maili Moja, Hamisi Salum Ally, amesema alikuwa anafuata maji mabondeni kwa ajili kufulia sare zake za shule lakini kutokana na kusogezewa huduma ya maji karibu imemsaidia kupata muda wa kujisomea.

Akizungumzia mradi huo, Mhandisi wa Maji Mji Kibaha, Grace Lyimo amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa wakazi wa Muheza ambapo ulikuwa na lengo la kuhudumia wananchi 911 lakini mpaka sasa unahudumia zaidi ya wananchi 2000.

"Mradi wa maji Muheza umejengwa kwa Shilingi Milioni 359 ambapo hutoa lita 100,000 kwa siku," ameongeza mhandisi Grace.

Mradi huo wa maji unaendeshwa na wananchi wa eneo hilo, ambapo hukusanya mapato ya mradi huo na kuziweka benki ambapo matumizi ya fedha hiyo ni pamoja na matengenezo madogo madogo ya mradi huo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi