Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wamachinga Arumeru Wagombania Vitambulisho vya Ujasiliamali
Jan 03, 2019
Na Msemaji Mkuu

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, akimkabidhi kitambulisho cha mjasiliamali mdogo mmoja wa wajasiliamali waliokidhi vigezo vya kupata kitambulisho hicho. Muro alikabidhi kitambulisho hicho baada ya kuzindua zoezi la ugawaji vitambulisho katika Wilaya ya Aruemeru. (Picha kwa Hisani ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru).

Na Mwandishi Wetu.

Wajasiliamali maarufu kama Wamachinga Wilayani Arumeru, wamemiminika kugombea vitambulisho vya ujasiliamali wakati Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro, akizindua rasmi zoezi la utoaji wa vitambulisho hivi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo  ambao mauzo ghafi hayazidi shilingi milioni nne.

Uzinduzi wa ugawaji vitambulisho hivyo umefanyika jana katika Halmashauri ya Arusha DC  eneo la Ngaramtoni na Halmashauri ya Meru katika eneo la Uwanja wa  Ngaresero na kuhudhuriwa na mamia ya wafanyabiashara ndogondogo ambao watanufaika na zoezi hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, akionesha kitambulisho cha mjasiliamali mdogo wakati wa uzinduzi wa ugawaji vitambulisho hivyo katika Wilaya ya Arumeru. (Picha kwa Hisani ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru).

Wilaya ya Arumeru inayoongozwa na Jerry Muro ina Halamashuri mbili za Arusha DC na Arumeru ambapo kwa kuanzia, Wilaya hiyo itatoa zaidi ya vitambulisho elfu sita kwa wafanyabiashara ndogondogo humo.

Mkuu wa Wilaya aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwainua kiuchumi na kuwaondolea adha ya kubugudhiwa mara kwa mara na ndio maana Rais Magufuli aliamua kuwatengenezea vitambulisho hivyo ili waweze kutambulika rasmi na kufanya biashara zao bila usumbufu.

"Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wafanyabiashara wadogo kama nyinyi na ndio maana Mheshimiwa Rais kaweka utaratibu wa kuwapatia vitambulisho na mimi Mkuu wenu wa Wilaya nitahakikisha wajasiliamali ambao mauzo yenu hayazidi milioni nne kwa mwaka mnapata vitambulisho hivi", alisisitiza Muro.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, akitoa maelekezo kwa baadhi ya wajasiliamali wadogo wakazi wa uzinduzi wa zoezi la kugawa vitambulisho vya wajasiliamali Wilayani humo. (Picha kwa Hisani ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru).

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilayani Arumeru, Musa Sudi, alisema kuwa TRA itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili waweze kutambua fursa zilizopo za kufanya biashara kupitia vitambulisho vya "Magufuli" hatua ambayo itawarahisishia ulipaji wa kodi pamoja na kuwasaidia kukua kibiashara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa zoezi la utoaji wa vitambulisho hivyo, Wakurugenzi wa Halmashauri za Arusha DC na Meru ,  Emanuel Mkongo pamoja na Dkt. Charles Mahela,  wamesema Halmashauri zimeweka utaratibu mzuri wa kuwatambua wafanyabiashara pamoja na kuwaratibu ili waweze kutambuliwa na kuingizwa kwenye mfumo rasmi ambao utatoa fursa ya wao kuweza kukua na kuepuka migongano ya mara kwa mara katika kufanya biashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi