[caption id="attachment_41307" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Mashtaka, Biswalo Mganga, akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) nakala ya hati ya mashtaka ya mauaji dhidi ya wakazi wawili wa Tabora ambao ilibainika wamebambikiwa na askari wa kituo cha Polisi Tabora baada ya ofisi yake kufanya uchunguzi. (Picha na Daudi Manongi-MAELEZO)[/caption]
Na ADELINA JOHNBOSCO, Habari Maelezo
Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imeeleza kuchukizwa na kitendo cha Polisi wilaya ya Tabora kuwabambikizia wananchi wawili kesi ya mauaji wakati wakijua ni uongo.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Biswalo Kachele Mganga, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, jijini Dodoma leo.
Kitendo cha kubambikiziwa kesi ya mauaji kilibainika baada ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya uchunguzi uliotokana na malalamiko kwenye barua ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, iliyochapishwa kwenye gazeti la Majira, toleo la tarehe sita ya mwezi Machi 2019.
“Baada ya kuisoma barua hiyo, mheshimiwa Rais aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo kwa haraka ili kujua ukweli wake”, anaeleza Mkurugenzi Biswalo.
Kwenye barua hiyo, mlalamikaji Musa Adam Sadiki alieleza jinsi askari wa kituo cha Tabora Mjini walivyomkamata na kumnyang’anya fedha kiasi cha Shilingi 788,000, simu ya mkononi na mali nyingine alizokuwa nazo kabla ya kumfungulia mashtaka ya mauaji kwenye Mahakama ya Tabora.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, baada ya kupitia nyaraka mbalimbali zikiwemo kitabu cha kuzuia wahalifu (detention register), ilibaninika mlalamikaji Musa Adam Sadiki alikamatwa tarehe 21 Juni, 2018 kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba, na kuwekwa mahabusu saa tisa alasiri siku hiyo hiyo.
Aidha, kitabu hicho kinaonesha kuwa tarehe 29 Juni, 2018 mlalamikaji alitolewa mahabusu na kufikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji ya Jackson Thomas yaliyotokea tarehe 6 Juni, 2018 barabara ya Kazima Tabora mjini, jambo ambalo lilibainika kuwa halina ukweli wowote.
Mbali ya kumbambikizia kesi ya mauaji Musa Adam Sadiki, pia ilibainika mkazi mwingine wa mji huo Edward Matiku aliyekamatwa tarehe 1 Julai, 2018 kwa kosa la kuvunja nyumba na kuiba ameunganishwa kwenye shauri hilo la mauaji namba 8/2018.
Kufuatia hatua hizo kukamilika, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Bw. Mganga, aliwafutia mashtaka yote na kuachiwa huru na mahakama tarehe 8 Machi, 2019.
Alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya mwendesha mashtka wa polisi aliyepeleka shauri hilo mahakamani wakati akijua kufanya hivyo ni kosa kutokana na ukweli kwamba mkoa wa Tabora unayo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, bwana Biswalo alisema tayari ameshamfuta kwenye orodha ya maofisa wa polisi waliokasimiwa mamlaka ya kuendesha mashauri ya jinai kwa niaba yake.
Zaidi Bw. Mganga ametoa rai kwa mawakili wote wa serikali wanaofanya kazi katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Waendesha Mashtaka wote nchini waliokasimiwa mamlaka ya kuendesha mashauri ya jinai na vyombo vya upelelezi kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila kumwonea mtu yeyote na kuzingatia maslahi ya taifa.
Wakati huohuo Rais Magufuli amempongeza bwana Sadiki kwa ujasiri aliouonesha kwa kuweka wazi malalamiko yake. Vile vile, mheshimiwa Rais amelipongeza gazeti la Majira kwa kutoa habari zenye ukweli, huku akivitaka vyombo vingine vya habari kuiga mfano huo.