Na: Mwandishi Wetu-MAELEZO
Zoezi la kuwarejesha wakimbizi raia wa Burundi waliohiari kurejea nyumbani limeanza leo ambapo jumla ya wakimbizi 301 wamerejeshwa nchini humo.
Zoezi hilo la kuwasafirisha limesimamiwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia wakimbizi (UNHCR), Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IMO) na washirika wengine wakiwemo Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) na Shirika la Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (IRC).
Msafara wa wakimbizi hao ambao wote wametoka kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo Mkoani Kigoma yenye wakimbizi 127,000 uliondoka kambini hapo saa nne asubuhi kwenda Mabamba mpakani mwa Tanzania na Burundi.
Katika eneo la Mabamba wakimbizi hao walipokelewa na viongozi wa Serikali ya Burundi na washirika mbalimbali wakiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Theranse Ndayiragije na wawakilishi wa shirika la UNHCR nchini Burundi.
Naibu Waziri wa Ndani ya Burundi katika maelezo yake kwa wakimbizi hao aliwahakikishia kuwa hali ya usalama ni nzuri na kuwa mali zao zikiwemo nyumba na ardhi zimehifadhiwa na watarejeshewa wenyewe watakapofika nyumbani.
Akizungumza na MAELEZO kwa njia ya simu kutoka mpakani wa Tanzania na Burundi Mkuu wa Mkoa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga alisema zoezi hilo limekwenda vizuri kama lilivyopangwa na wakimbizi waliorejea walionesha furaha kwa kupata fursa ya kwanza kurejea.
Mkuu wa Mkoa huyo alibainisha kuwa taarifa za hivi karibuni zinaonesha kuwa wakimbizi zaidi ya 6,000 wa kambi ya Nduta wamejiandikisha kurejea nyumbani wakiwa ni miongoni mwa wakimbizi 12,000 wa nchi hiyo waliojiandikisha kwa hiari hadi sasa kurejea nchini Burundi.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Wakimbizi kanda ya Kigoma Tonny Laizer, zoezi hilo litaendelea tena Jumane ijayo tarehe 12 Septemba, 2017 ambapo litajumuisha wakimbizi 350.
Hivi sasa kuna wakimbizi raia wa Burundi 256, 850. Zoezi hilo linafanyika kufuatia kutiwa saini makubaliano ya kuwarejesha wakimbizi hao kati ya Serikali za Tanzania, Burundi na shirika la UNHCR hivi Karibuni jijini Dar es Salaam.