Na Benny Mwaipaja,WFM, Simiyu
ZAIDI ya Wakazi elfu 2 wa Mji wa Lagangabilili, Tarafa ya Kanadi, Wilayani Itilima, mkoani Simiyu, wameondokana na adha ya kukosa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi wa maji ya bomba wa Lagangabilili uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 900.
Wakizunguza mbele ya timu maalumu ya wataalam wanaofuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka baadhi ya Wizara wakiongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Baadhi ya wakazi wa Mji huo wa Lagangabilili wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi huo wa maji.
"Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea maji tunayapata kwa urahisi, zamani tulikuwa tukihangaika sana akina mama walikuwa wakiyafuata mto Simiyu, mbali sana, walikuwa wakitoka saa kumi usiku na kurudi saa tatu asubuhi" alisema Bw. Chonza Maduhu, mkazi wa Lagangabilili, Simiyu
Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Itilima, Bw. Goodluck Masige, amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumefanya kiwango cha upatikanaji maji safi na salama kwenye mji huo ambao ndio makao makuu ya wilaya ya Itilima, kupanda kutoka asilimia 20 za awali hadi kufikia asilimia 100.
"Tumejenga tenki lenye ujazo wa lita 225,000, vituo 21 vya kuchotea maji, tumejenga mtandao wa bomba za kusambaza maji nyenye urefu wa mita 29,000 na kufunga pampu 1 ya kusukuma maji" aliongea Mhandisi Masige
Ameitaja kazi iliyosalia kukamilisha mradi huo unaotarajiwa kukabidhiwa Serikalini na mkandarasi, Kampuni ya M/S Nangai Contractors and Engineering Co. Ltd, Disemba 30, 2018, kuwa ni ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo (Cattle trough) ( Pause: Mhandisi Goodluck Masige-Mhandisi wa Maji Wilaya ya Itilima
Mmoja wa Wajumbe wa timu ya Kitaifa ya ufuatiliaji wa miradi ya maji katika mikoa ya Simiyu na Mara, Bw. Jordan Matonya, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa maeneo mbalimbali nchini inatekelezwa kwa viwango vya hali ya juu na kuwanufaisha wananchi.