Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameridhika na uwekezaji wa kilimo cha miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari katika kata ya Mvuha iliyopo Morogoro Vijijini ambapo kampuni ya Morogoro Sugar inataraji kuwekeza.
Akizungumza wakati wa mkutano wa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji tisa vilivyopo katika kata ya Mvuha Wilaya ya Morogoro vijijini Waziri Lukuvi amesema uwekezaji huo ambao unataraji kuchukua ekari 92,000 ambapo mwekezaji atapewa ekari 10,000 na wazawa ekari 82,000 ili kulima miwa na kuzalisha sukari.
Aidha suala hilo limekuja baada ya kuwepo kwa mgogoro uliodumu kwa miaka nane tangu mwaka 2011 kati ya wananchi wa maeneo hayo na mwekezaji wa kiwanda hicho suala ambalo limetatuliwa mbele ya Waziri Lukuvi.
Hata hivyo Waziri Lukuvi ameeleza faida zitakazopatikana kuwepo kwa mwekezaji huyo ni pamoja na wananchi kupata ajira kwenye mashamba hayo, huku wengine wakinufaika na ajira za kiwandani hivyo kuongeza pato katika halmashauri zao.
“Mwekezaji atatoa elimu juu ya kilimo cha miwa pamoja na kuwezesha miradi mbalimbali ikiwemo nyenzo za kilimo kama mikopo na matrekta, utaalamu, mbegu na mbolea lakini baada ya hapo hizo gharama zitakokotolewa, mtakatana wakati wa mauzo na nyinyi mtakuwa na zao la kudumu sababu soko litakuwa hapahapa” amesema Waziri Lukuvi.
Aidha Waziri Lukuvi ametoa wito kwa wanakijiji kutenga hekali elfu 82 watakayoitumia wakulima wa wanje ya shamba la muwekezaji ambapo kila mkulima atakuwa na shamba lake kwani hekali elfu kumi alizopewa muwekezaji hazitoshi.
Pia Waziri Lukuvi ametoa wito kwa viongozi wa vijiji kushirikiana na wawekezaji wanaojitokeza kuwekeza katika vijiji vyao ili kuongeza thamani ya ardhi kutoka kuwa mashamba pori na kuwa ardhi itakayo waletea manufaa.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Tununguo ndug. Bonas Thomas Ndonga amemuomba Mwekezaji kutengeneza daraja linalounganisha kijiji cha Ngerengere na Tununguo ili kuwepo kwa mawasiliano kati ya vijiji hivyo.