Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wafanyabiashara, Wakulima Wasifia Uwepo Soko la Mazao ya Nafaka Makambako
Jan 18, 2024
Wafanyabiashara, Wakulima Wasifia Uwepo Soko la Mazao ya Nafaka Makambako
Muonekano wa soko la mazao ya nafaka lililopo katika eneo la Kihumba
Na Jacquiline Mrisho - Maelezo

Wafanyabiashara, wakulima na wanunuzi wa mazao ya nafaka Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe wamesifia uwepo wa soko la mazao hayo lililopo katika eneo la Kihumba kwa kuwarahisishia mnyororo mzima wa biashara hiyo kuanzia kwenye uletaji, utunzaji, ununuaji na uuzaji.

Zakaria Chaula ambaye ni Mfanyabiashara wa Mazao ya Nafaka katika soko hilo amesema kuwa awali kabla ya soko hilo la pamoja, walikuwa wanafanya biashara ya mazao ya nafaka katika makazi ya watu ambapo kila mfanyabiashara alikuwa anatafuta eneo lake analoona linamfaa kwa biashara.

Ameongeza kuwa, maeneo hayo yalikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa maeneo ya kuegeshea magari kwa ajili ya kushushia au kupakia mizigo, kupima mizigo kienyeji kwa kutumia ndoo na mizigo kutokupimwa ubora.

"Katika Halmashauri hii, wafanyabiashara ambao tulikuwa hatuna soko la pamoja ni sisi wauza mazao ya nafaka, hivyo tunaishukuru Serikali kwa kutuwezesha na sisi kupata sehemu moja ya kufanyia biashara zetu kwani kupitia soko hili kumekuwa na ongezeko la wateja hasa wa kutoka nchi za nje kwa kuwa mazao yote yako sehemu moja, soko lina wataalam wa kupima ubora wa mazao na kupima kiasi kwa kutumia mizani, pia wakulima wanauza kwa bei za pamoja hivyo kuwasaidia wakulima kutokuuza kwa hasara," alisema Chaula.

Kwa upande wake mkulima anayeleta mazao ya nafaka kwa wafanyabiashara kutoka shambani, Khalid Chengula amesema kuwa kabla ya soko hilo ilikuwa ni changamoto kwao wakulima kuwatafuta wateja wa mazao hayo wakileta mizigo sokoni kwa sababu wafanyabiashara hawakuwa wanakaa katika eneo moja hivyo kupelekea kutumia fedha nyingi kwa kukaa muda mrefu mjini kutafuta wateja walipo pamoja na kutumia gharama kubwa za mafuta ya gari kutokana na wateja kuwa maeneo tofauti tofauti.

"Kwa sasa wakulima tunauza mazao yetu kwa bei inayoridhisha kwa sababu tunauza sehemu moja tofauti na mwanzo kila mkulima alikuwa anauza kutegemea na maelewano na mfanyabiashara mmoja mmoja," alisema Chengula.

Naye mmoja wa wanunuzi, Marietha Mzava amesema kuwa ni kweli changamoto zilikuwa nyingi ikiwemo kutumia muda mrefu sokoni kwenye uchaguzi wa nafaka bora kwa kuwa wauzaji walikuwa mbalimbali pamoja na changamoto ya ubebaji wa mizigo baada ya kununua lakini sasa Serikali imerahisisha wananchi wanapata nafaka sehemu moja bila kutumia muda mrefu.

Kwa upande wake Afisa Biashara wa Halmashauri ya Mji Makambako, Carlos Mhenga amesema kuwa lengo la kuanzisha soko hilo ni kupanga mji na kuwa na soko kuu ambalo ni rasmi kwa ajili ya kuhifadhi na kuuza mazao ambapo kupitia soko hilo, halmashauri itaweza kutambua mzunguko wa biashara  ya mazao kwa kujua kiasi kinachotoka na kinachoingia.

"Ujenzi wa soko hili ulianza tangu mwaka 2018 ambapo ujenzi wa maghala ulikadiriwa kuwa 2,120,000,000 ambapo mpaka sasa zimeshatumika shilingi 1,200,000,000. Hata hivyo, kuna ujenzi wa vizimba 587 uliokadiriwa kugharimu shilingi 129,140,000 ambao ujenzi wake unaendelea," alisema Mhenga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi