Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Jumla ya Vijiji 75 vilivyokuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi katika Mkoa wa Arusha vimenufaika na hisani ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kwake kubaki maeneo yake kufuatia vijiji hivyo kuingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi.
Mkoa wa Arusha unahusisha vijiji na mitaa 116 kati ya 975 vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi na hifadhi, mashamba, ranchi, mapori ya akiba na vyanzo vya maji ambapo taarifa yenye mapendekezo ya utatuzi wake iliwasilishwa serikalini tarehe 23 Septemba, 2019 na kutolewa uamuzi na Baraza la Mawaziri.
Katika taarifa hiyo ilipendekezwa vijiji 920 kati ya 975 vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi nchini kubaki ingawa baadhi yake vitahusisha marekebisho ya mipaka kwa njia shirikishi na baadhi yake migogoro yake ilishatatuliwa.
"Vijiji na mitaa 116 Arusha kuachiwa vijiji 75 kubaki kwenye maeneo yake ni hisani ya kipekee na tunatakiwa tuiheshimu na tusiitumie vinginevyo kwa sababu Mhe. Rais Samia alikuwa na uwezo wa kuviondoa lakini ameridhia maeneo 75 kubaki", alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula.
Akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Arusha tarehe 20 Aprili, 2022 wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta mkoani humo, Dkt. Mabula alisema, sambamba na uamuzi wa Serikali, uongozi wa mkoa utakuwa na jukumu la kusimamia mpango wa matumizi ya ardhi sambamba kudhibiti vyanzo na vichocheo vyote vya kuzalisha migogoro.
"Natambua Mkoa wa Arusha una changamoto nyingi zinazosababishwa na muingiliano wa matumizi ya ardhi lakini niwakumbushe kuweka utaratibu mzuri wa utekelezaji na uamuzi wa serikali unaohusu migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 nchini", alisema Dkt Mabula.
Kwa upande wao, Mawaziri wa Wizara za Kisekta walihimiza umuhimu wa viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi chini kusimamia vyema utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila kuleta taharuki kwa wananchi sambamba na kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanatunzwa.
“Kama Wizara ya Kilimo tupo katika mchakato wa kutunga sheria ya kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kutenga na kubaini maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za kilimo ili kuondoa migogoro ya ardhi”, alisema Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega alisema, uzoefu unaonesha kuwa maeneo mengi yaliyoathirika na uvamizi ni ya mifugo na kusisitiza kuwa maeneo hayo ni ranchi zinazotumika pia kama ardhi ya akiba na kuweka wazi kuwa, hakuna namna yoyote maeneo hayo kutoonekana vichaka.
Tayari Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta katika awamu ya pili ya kupeleka mrejesho wa maamuzi ya baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 imeshatembelea Mikoa ya Pwani, Morogoro, Tanga, Mara na Arusha.