Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha kwanza nchini kitakachojihusisha na utengenezaji wa vifaa vinavyotumika kuunganisha mifumo ya umeme, maarufu kwa jina la kigeni kama ‘insulators.’
Aliweka jiwe hilo, Agosti 10, 2020 katika eneo la kiwanda cha Inhemeter, Kinondoni jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyowashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyakazi wa kiwanda husika na baadhi ya wananchi.
Katika hotuba yake aliyoitoa muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi, Dkt Kalemani alitoa pongezi kwa uongozi wa kiwanda hicho, kuitikia wito wa Serikali, uliotolewa kwa wawekezaji kuanzisha viwanda mbalimbali nchini.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuweka será, dira na mwelekeo madhubuti wa kujenga uchumi wa viwanda akisema ndivyo vilivyowezesha wawekezaji mbalimbali kuendelea kuanzisha viwanda nchini.
“Hili ni tukio muhimu sana. Kwa mara ya kwanza hapa nchini, tunazindua Mradi wa aina hii. Pongezi nyingi kwa Serikali na hongereni sana uongozi wa kiwanda.”
Akielezea jitihada zilizofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati, katika kuhakikisha vifaa mbalimbali vya umeme vinatengenezwa nchini na kuachana na kasumba iliyozoeleka ya kuagiza kutoka nje, Dkt Kalemani alisema mkakati huo umekuwa ukitekelezwa hatua kwa hatua na umekuwa wenye mafanikio.
Alisema hatua ya kwanza ilikuwa mwaka 2017 ambapo Serikali iliweka zuio la kuleta baadhi ya vifaa vya kuunganishia umeme kama vile nguzo, kutoka nje ya nchi.
“Leo viko viwanda 13 vya kuzalisha nguzo za umeme hapa nchini kutoka kiwanda kimoja tu kilichokuwepo awali,” alieleza.
Waziri alifafanua kuwa, hatua ya pili ilifanyika mwaka 2018 kwa Serikali kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha mita za umeme, ambapo alitoa shukrani kwa kampuni ya Inhemeter na Baobab, ambao walianza kujenga viwanda hivyo.
Alisema, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuweka zuio la kuagiza nyaya za umeme kutoka nje ya nchi, ambapo kufuatia hatua hiyo, hadi sasa kuna viwanda vinne vya kuzalisha nyaya hizo hapa nchini, kutoka kiwanda kimoja cha TANALEC kilichokuwepo awali.
Akieleza zaidi, Waziri alisema baada ya hapo alitoa maelekezo kwamba ifikapo Oktoba 2020, Serikali haitaruhusu kuingiza vifaa vya viunganishi kutoka nje ya nchi badala yake vizalishwe hapa nchini.
“Nashukuru Oktoba bado haijafika. Leo ni mwezi wa nane ambapo tunafungua kiwanda hiki cha kuzalisha viunganishi. Hongereni sana,” alipongeza Waziri.
Waziri Kalemani, alitumia fursa hiyo kusisitiza msimamo wa Serikali kwamba, kuanzia sasa, hakuna ruksa kwa kifaa cha aina yoyote kinachotumika kusambaza umeme, kitakachoruhusiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi, hususani kwa miradi inayotegemea fedha za Serikali.
Aidha, alieleza kufarijika na taarifa aliyopewa na uongozi wa kiwanda cha Inhemeter kuwa, wanatarajia siku za usoni, kuanza uzalishaji wa nyaya maalumu zinazotumika kupitisha umeme ardhini na chini ya maji.
Waziri aliwahakikishia wawekezaji hao soko la uhakika la bidhaa zao lakini akawatahadharisha kuwa wasitumie mwanya huo kupandisha bei bali waweke bei zenye ushindani wa soko.
Katika hatua nyingine, alisema uunganishaji umeme vijijini umefikia vijiji 9,512 kati ya 12,257 vilivyopo nchi nzima. Aliongeza kuwa, kuanzia tarehe 20 Agosti hadi 20 Septemba, 2020, Serikali itaanza kupeleka wakandarasi watakaofanya kazi ya kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji vyote vilivyosalia.
“Niwatoe hofu wananchi ambao vijiji au vitongoji vyao havijafikiwa na umeme kwani wote watafikiwa kabla ya Juni 2021. Pesa za kutekeleza Mradi huo tunazo ambapo jumla yake ni takribani shilingi bilioni 851.”
Awali, akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Kalemani, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo, alishukuru na kupongeza jitihada za Serikali kupitia sekta ya nishati, zilizowezesha uwekezaji katika maeneo mbalimbali, kutokana na kuwepo uhakika wa upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Abrahamu Rajakili alisema kitaajiri watanzania takribani 120 na kwamba kina uwezo wa kuzalisha viunganishi milioni 1.5 kwa mwaka, huku kikilenga soko la ndani na nje ya nchi.
Kiwanda cha Inhemeter kimekuwa kikizalisha mita za umeme kabla ya kuwekeza takribani shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuanza kuzalisha viunganishi vya mifumo ya umeme.