Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uunganishwaji Mamlaka Ndogo za Maji Kupunguza Changamoto za Utendaji Kazi
Mar 06, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_41117" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akizungumza leo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Maji nchini unaolenga kuwaelimisha wadau hao kuhusu uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini.[/caption]

Na Jacquiline Mrisho

Uunganishwaji wa Mamlaka ndogo za maji zilizopo katika miji midogo nchini kwa nia ya kuhudumiwa na Mamlaka za Maji za Mikoa husika unategemewa kupunguza changamoto za utendaji kazi zinazotokea katika maeneo hayo.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Maji nchini unaolenga kuwaelimisha wadau hao kuhusu uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini.

Prof. Mbarawa amesema kuwa katika Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira kuna kitu kinaitwa ‘Cluster’ ambapo Mamlaka za Maji za Mikoa zitasimamia Mamlaka ndogo ndogo zilizopo chini ya mkoa husika hali itakayosaidia upatikanaji wa huduma za maji Mijini na Vijijini kuwa sawa.

“Kwa vile sheria imeruhusu uunganishwaji huo, Mamlaka za Maji zinaweza kujitanua, kufanya biashara nzuri, kuongeza kipato na kupunguza changamoto za utendaji kwa sababu baadhi ya maeneo yamewekwa mitambo mikubwa lakini Mamlaka husika ni ndogo haziwezi kuendesha kazi hizo,” alisema Prof. Mbarawa.

[caption id="attachment_41118" align="aligncenter" width="1000"] Baadhi ya Wadau wa Maji wakimsikiliza Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho.[/caption]

Vile vile ametoa rai kwa mamlaka hizo kutojiweka mijini pekee na badala yake zijikite zaidi katika kuongeza kasi ya utoaji huduma za maji hata nje ya miji husika.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa pamoja na jitihada kubwa za kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) utendaji kazi wake ni kitu kingine hivyo, watendaji wanatakiwa kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa ya kupeleka huduma za maji vijijini yanatekelezeka.

“Ili kuhakikisha huduma za maji zinafika katika maeneo husika, wataalam wa sekta ya maji lazima tubadilike kuhusu suala la kuandaa miradi kwani Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuhakikisha wananchi hasa wa vijijini wanapata maji lakini miradi inamalizika na maji hayatoki, hilo sio jambo zuri na sio mpango wa Serikali,” alisema Aweso.

Aidha, Aweso ametoa rai kwa wadau wa sekta hiyo kuchagua wakandarasi wenye uwezo wa kutekeleza miradi na kuikamilisha kama ilivyopangwa ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo na wananchi wanapata huduma iliyokusudiwa.

[caption id="attachment_41119" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa na baadhi ya Wenyeviti wa Bodi za Mamlaka za Maji wakisainishana mkataba wa utendaji kazi utakaosaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya maji katika ngazi mbalimbali nchini mara baada ya kufungua kikao hicho. Mikataba hiyo itakua ikipimwa na Wizara husika kila mwaka.[/caption] [caption id="attachment_41120" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya maji mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa Wadau wa Maji nchini unaolenga kuwaelimisha wadau hao kuhusu uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini.[/caption]

Mkutano huo umehusisha wadau wa sekta ya maji wakiwemo watumishi kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Maji na Nishati (EWURA), Mabonde ya Maji, Wakala wa Uchimbaji Visima, Mfuko wa Maji pamoja na Chuo cha Maji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi