Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Utoaji wa Taarifa za Miradi ya Maendeleo kwa Wananchi ni Takwa la Kisheria- Dkt. Abbasi
Mar 16, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Frank Mvungi- Mwanza

Watendaji Wakuu wa Serikali katika ngazi mbalimbli wametakiwa kutoa taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa maeneo husika ili kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza ushirikishaji.

Akizungumza wakati wa mahojiano maalum leo Jijini Mwanza, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawataka Viongozi wote kuhakikisha wananchi wanapata taarifa za miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

 “Kutoa taarifa kwa wananchi ni takwa la Kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria Na 12 ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, hivyo kila Kiongozi ahakikishe kuwa wananchi wanapata taarifa za utekelezaji wa sera na miradi yote inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi” Alisisitiza Dkt. Abbasi.

Akizungumzia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano Dkt. Abbasi amesema kuwa kwa sasa dhamira ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na maisha bora kutokana na dhamira safi ya Serikali ya Awamu ya Tano kulenga kuwakwamua wananchi wanyonge kiuchumi.

Serikali inatekeleza miradi ya kimkakati ya; mradi wa kufua umeme wa mto rufiji, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa hospitali za Wilaya 67, ununuzi wa ndege sita (06) ambazo tayari zimenunuliwa ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanafikiwa kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi wote.

Mkurugenzi Abbasi ameitaja miradi mingine ya ujenzi wa vivuko, meli mpya na za kisasa  ambapo tayari bilioni 20 zimetolewa na Serikali kwa ajili kutekeleza kujenga meli, ujenzi wa uwanja changamani na wa kisasa kwa ajili ya kukuza sekta ya michezo eneo la Nane nane jijini Dodoma.

“Miradi yote inayotekelezwa na Serikali imekuwa chachu ya maendeleo na imekuwa chanzo cha kuzalisha ajira kwa wananchi hasa Vijana lengo ni kuhakikisha kuwa wanaiunga mkono Serikali ili azma yakuwaletea maendeleo itimie kwa wakati”. Alisisitiza Dkt. Abbasi.

Katika Kuboresha sekta ya Elimu Serikali ya Awamu ya Tano inatoa zaidi ya bilioni 23 kila mwezi kugharamia elimu bure ili kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo hapa nchini kwa kuzingatia umuhimu wa suala la elimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Bw. Paschal Shelutete amesema kuwa  Maafisa Habari wote  Tanzania wanakutana Jijini Mwanza kwa mkutano mkuu wa Mwaka utaoanza Jumatatu Machi 18 hadi 22, 2019 kwa lengo la kujengewa uwezo Maafisa hao ili kuisemea Serikali katika kuwaeleza wananchi utekelezaji wa miradi inayetekelezwa na Serikali katika maeneo yao.

“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kujali na kuona umuhimu wa Kada ya Mawasiliano Serikalini na kuweka mkazo katika kuimarisha sekta hii kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla” Alisisitiza Shelutete.

Akifafanua hayo, Shelutete amesema kuwa wakati wa mkutano huo Maafisa Habari watajengewa uwezo na kupewa mbinu za kisasa katika kuisemea Serikali katika maeneo yao zikiwemo Wizara,  Mikoa, Wilaya, Majiji, Halmashauri, Taasisi, Wakala, Idara zinazojitegemea kote nchini.

Kikao Kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano kitafanyika Jijini Mwanza kuanzia machi 18-22, 2019 na kinatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa. Mahojiano na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Dkt. Hassan Abbasi pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamefanyika leo machi 15, 2019 Jijini Mwanza wakati wa ziara yao ya kutembelea vyombo vya habari Jijini humo.

     

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi