Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ushirikiano Ndio Njia Muhimu Katika Kupata Takwimu Sahihi - Makamba
Mar 26, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Adelina Johnbosco: MAELEZO, Dodoma

Tanzania ili iweze kufikia hatima ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi , ofisi ya Taifa ya takwimu ishirikiane vyema na taasisi pamoja na mashirika ya utafiti katika kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoa takwimu sahihi.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba wakati wa uzinduzi wa semina ya wadau kuhusu uanzishwaji wa ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa wa uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa takwimu za mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.

''Ripoti zifanane, vitu vyote vyaweza kuharibiwa lakini sio takwimu, kwani ndio kioo cha kila jambo duniani, utofauti ukionekana kwenye ripoti itakwamisha wadau na serikali kwenye mipango ya maendeleo,'' amesema Makamba

Mbali na ushirikiano, amesisitiza watafiti kujengeana uwezo katika kuhifadhi na kuchambua takwimu ili kufikisha ujumbe kwa walengwa, kwani uchambuzi huo huchangia maamuzi sahihi ya mipango ya maendeleo.

Aidha, ameitaka ofisi ya Taifa ya Takwimu na wadau wengine wa kitaifa na kimataifa katika masuala ya tafiti kuhusu mazingira, wajikite katika kutoa elimu kwa umma juu ya visababishi na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kwani uhafifu wa uelewa juu ya mazingira unasababisha wananchi kuwa vyanzo vikuu vya tatizo.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, amesema lengo kuu la takwimu za tafiti juu ya mazingira ni kuhakikisha zinapatikana taarifa rasmi ili kuwasaidia watunga sera nchini na duniani kote katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

"Kama takwimu zikiwa sahihi, na za kutosha, tatizo la tabia ya nchi litakomeshwa kwani hakutakuwepo na mkanganyiko wa kujiuliza ni nini sababu kuu ya tatizo wakati kila kitu kitakuwa wazi," amesema Dkt. Chuwa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Taifa cha Takwimu Benedict Mugambi, akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, amesema, kuna uhusiano mkubwa kati ya watu, mazingira na uwepo wa mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo watu wanapaswa kuelimishwa juu ya utunzaji wa mazingira mahali wanapoishi.

''Katika sensa ya watu na makazi sehemu yenye watu wengi kuna uharibifu zaidi wa mazingira unaopelekea uwepo wa mabadiliko ya tabia ya nchi kuliko penye watu wachache,'' amesema Mugambi

Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Serikali ya Ujerumani (GIZ), Samwel Sudi amesema takwimu za mazingira zikitumika vyema zinachagiza uwepo wa maendeleo, kwani taarifa hizo zinasaidia wadau wa maendeleo na serikali kutekeleza mambo mbalimbali yanayohusu mabadiliko ya tabia ya nchi.

''Tunajitahidi kuweka mikakati ya kuhakikisha ulimwenguni kote tunakuwa na njia za kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko mbalimbali ya nchi ikiwemo mafuriko, ukame na hewa chafu, hii itasaidia kuwepo kwa maendeleo katika nyanja zote'' amesema Victor Ohuruogu Mwakilishi kutoka Ushirikiano wa Kimataifa wa Takwimu kwa Maendelelo Endelevu (Global Partinership for Sustainable Development Data- GPSDD)

Suala la mazingira na hali nzuri ya tabia ya nchi si la nchi moja pekee, wakati Tanzania ikiweka mikakati ya kutumia takwimu kukabiliana nalo, wadau wa kimataifa nao wanalipigania kuhakikisha duniani kote hali inatengamaa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi