Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ushirikiano kati ya Tanzania na India Kuenziwa : Dkt. Mwakyembe
Jan 16, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na. Grace Semfuko-MAELEZO

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema ushirikiano wa kiutamaduni na kihistoria uliopo baina ya Tanzania na India unaotokana na Waasisi wa haki, usawa na amani wa Mataifa hayo akiwepo Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Mahatma Gadhi wa India hivyo ni muhimu kuenziwa.

Waziri Mwakyembe aliyasema hayo Jijini Dar Es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Picha halisi za maisha ya Mwasisi wa India Mahatma Gandhi yajulikanayo kama “MahatmaGandi kupitia lensi za Kanu Gandhi” yenye lengo la kuenzi juhudi zake za kuleta usawa,kuboresha na kuendeleza jamii, usafi,fikra za kukuza uchumi, upendo na kuimarisha mazingira.

Mwakyembe alisema historia za Tanzania na India katika kudai uhuru zinalingana kutokana na waasisi wa mataifa haya kutumia njia za kidiplomasia bila kumwaga damu hali ambayo inapaswa kuenziwa na kupongezwa.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwanafunzi wa Gandhi, kiongozi huyu aliishi maisha  ya kawaida kabisa,kwetu sisi  wananchi wa Tanzania huu ni mfano wa kuigwa kwani  hatua ya kupata Uhuru wetu  ingekuwa kwa nchi zingine ilihitaji kupigana, lakini Mwalimu  Nyerere aliudai uhuru taratibu na bila kumwaga Damu  kama ambavyo India chini ya Mahatma Gandhi ilivyodai uhuru bila kumwaga damu, hivyo basi maonesho haya tunayapa umuhimu mkubwa sana na inaonyesha urafiki mkubwa katika nchi hizi mbili” alisema Waziri Mwakyembe.

Kiongozi huyo wa India Mahatma Gandhi alizaliwa miaka alizaliwa miaka 150 iliyopita na kufariki miaka 70 iliyopita, anasifiwa kwa kuishi maisha ya kawaida, kupigania haki, uhuru na usawa wa Taifa la India, anajulikana kuwa ni mtu wa kipekee kiongozi wa siasa wa kidunia mwenye mvuto katika viongozi wakuu wa karne ya 20.

Umoja wa mataifa UN wanatambua ujumbe wa Mahatma wa ukweli na kuepuka matumizi ya nguvu na kuamua kuitangaza siku ya kimataifa ya kutotumia nguvu katika kudai haki lengo likiwa ni kuenzi na kujali utu na kuimarisha fikra za kukuza uchumi katika mataifa mbalimbali Duniani.

Dkt Mwakyembe alisema kuwa mahusiano maalum ya Gandhi kwa  Afrika yalitambuliwa na Waziri Mkuu wa zamani Dkt Salim Ahmed Salim na kwamba ni mfano wa kuigwa kwa nchi hizo.

Balozi wa India Nchini Tanzania Sandeep Arya alisema wameamua kufanya maonesho hayo ili kuenzi juhudi za Mahatma za kuimarisha usawa bila kujali tofauti za rangi na makabila huku lengo likiwa ni kuimarisha utu na uchumi baina ya Tanzania na India.

“Mahatma aliweza kupigania usawa, maonesho haya ni ishara tosha kuwa Tanzania na India tupo katika mstari mmoja kwenye jambo hili, lengo ni kuleta ujumbe wa kuimarisha usawa na kuimarisha uchumi” alisema Balozi Sandeep Arya.

Naye Balozi wa Afrika Kusini Nchini Tanzania Bw.Thamsanga Dennis Mseleku alisema Mahatma alikuwa mfano wa kuigwa kwenye nchi yake kutokana na kuweza kujifunza mengi kutoka kwake ikiwepo kuondokana na ubaguzi wa rangi, ukabila pamoja na kudai uhuru.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi