Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Upatikanaji wa Dawa na Vifaa Tiba Wafikia Zaidi ya Asilimia 90 Mtwara
Dec 20, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi wetu

  Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Hospitali, Vituo vya vya afya na Zahanati zote mkoani Mtwara umefikia zaidi ya asilimia 90 katika kipindi cha miaka 4 ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa amesema kuwa upatikanaji wa dawa unaenda sambamba na kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea huduma  kama majengo mapya  na vifaa tiba.

“Vituo vya afya 13 vimejengwa  na 9 kati yake vimeanza kutoa  huduma na pia Hospitali 3 za wilaya zimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.5 ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuimarisha huduma za afya katika Mkoa wa Mtwara,” alisisitiza Byakanwa.

Akifafanua amesema kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda inajengwa katika mkoa huo na itahudumia wananchi wa mikoa yote ya Kanda ya Kusini hasa kwa kuhakikisha kuwa huduma za kibingwa zinatolewa kwa wananchi hao kwa tija.

Akizungumzia upatikanaji wa maji mjini Mtwara umefikia asilimia 82  kwa sasa na upande wa vijijini  umefikia asilimia 55 ambapo unatarajiwa kuongezeka maradufu kutokana na miradi mingi inayoendelea kutekelezwa katika wilaya zote katika mkoa huo.

Kuhusu sekta ya elimu Byakanwa amesema kuwa shilingi bilioni 8 zimetumika kukarabati Chuo cha Ualimu Kitangali wilayani Newala mkoani Mtwara pamoja na ujenzi wa miundombinu kama madarasa , maabara na vyoo katika shule za sekondari na msingi .

Kuimarishwa kwa miundombinu katika sekta ya elimu kumechangia kukuza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 65 hadi asilimia 82.

Kipindi cha TUNATEKELEZA kinaratibiwa na Idara ya Habari( MAELEZO) na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na awamu hii inawashirikisha wakuu wa mikoa wote Tanzania Bara.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi