Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeeleza kuwa, kazi ya uletaji wa mafuta kwa pamoja nchini inayosimamiwa na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ina tija kwa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ikwemo ya nchi kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta ikiwemo dizeli na petroli.
Hayo yamesemwa na Wajumbe wa Kamati hiyo baada ya kukagua miundombinu ya kushusha na kupima mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na hifadhi kubwa ya mafuta ya kampuni ya TIPER ambayo Serikali ni mbia kwa umiliki wa hisa asilimia 50.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mha.Felchesmi Mramba ilifanyika tarehe 14 Novemba, 2022, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japhet Hasunga alisema kuwa, lengo la ziara lilikuwa ni kuona uwezo wa miundombinu hiyo katika kushusha na kuhifadhi mafuta.
Mhe. Hasunga alieleza kuwa, baada ya ukaguzi huo Kamati hiyo imejihakikishia kwamba miundombinu iliyopo ya ushushaji na uhifadhi mafuta ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya nchi hivyo Kamati hiyo imefurahishwa na uwepo wa miundombinu hiyo.
Hata hivyo, Kamati hiyo ilitoa wito kwa TIPER kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta katika maeneo mengine ya nchi ili kuongeza uwezo wa kampuni na nchi katika kuhifadhi mafuta na pia kuleta urahisi katika usafirishaji wa mafuta hayo ndani na nje ya nchi.
Awali, kabla ya kufanyika kwa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi, aliieleza Kamati hiyo kuwa, kutoka Wakala huo uanzishwe mwaka 2015 umekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji na yenye viwango vya ubora unaohitajika.
Manufaa mengine ni Serikali kuweza kupanga ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia takwimu sahihi, kuweza kupanga bei elekezi ya mafuta pamoja na kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta nchini kutokana na uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa wastani wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 200 Sawa na Shilingi bilioni 462 huokolewa kwa mwaka.
Aidha, alisema kuwa, kutokana na mfumo huo kuleta ufanisi, nchi za jirani pia zinatumia mfumo huo kuagiza mafuta kupitia Tanzania hivyo kuipatia Serikali mapato kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya bandari.
Aliongeza kuwa, mfumo huo umesaidia kupunguza upotevu wa mafuta wakati wa kupakua mafuta kutoka melini ambapo wastani wa Tani 1100 (lita 1,300,000) huokolewa kila mwezi sawa na Shilingi bilioni 4.3.