Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi Mji wa Serikali Wakamilika 99%
Mar 27, 2019
Na Msemaji Mkuu

 

 

[caption id="attachment_41448" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza na uongozi na watumishi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (hawapo pichani) baada ya kukagua ujenzi wa jengo la wizara hiyo kwenye mji wa Serikali Ihumwa, Dodoma. Waziri Mkuu Majaliwa amewapongeza watumishi na viongozi wa wizara hiyo kwa kukamilisha ujenzi ndani ya muda. Pembeni ya Waziri Mkuu ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa na katikati ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Francis Michael[/caption]

Na. Immaculate Makilika-MAELEZO 

Ujenzi wa majengo ya Wizara kwenye Mji wa Serikali uliopo Ihumwa jijini Dodoma umekamilika kwa asilimia 99 ambapo wizara 20 zinatarajia kuhamia ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.

Akizungumza leo mara baada ya kufanya ziara  katika mji huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa ujenzi kwenye mji huo umekamilika kwa asilimia 99, aidha amezitaka wizara hizo kukamilisha sehemu ndogo zilizobaki kabla ya mwezi Aprili mwaka huu, ikiwa ni baada ya kupata hati kutoka Wakala wa Ujenzi (TBA).

Waziri Mkuu Majaliwa amesema, “kwa ujumla kazi ni nzuri na imefanywa kwa umakini mkubwa, jukumu lililobaki ni kuhakikisha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaweka umeme wenye nguvu na wakutosha, barabara zote zipitike kwa urahisi, na lazima kuwepo na huduma muhimu ikiwemo kituo cha afya, hoteli, stendi ya daladala na maduka ili watumiaji wa majengo haya waweze kupata huduma hizo”.

[caption id="attachment_41449" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa msimamizi wa ujenzi wa majengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Katiba na Sheria kwenye eneo la Mji wa Serikali Ihumwa, Dodoma wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo leo. Waziri Mkuu amempongeza mkarandasi SUMA JKT kwa kukamilisha majengo ya wizara hizo tatu ndani ya muda kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa ujenzi.[/caption]

Vile vile ameagiza Makatibu Wakuu wa wizara zote kuhakikisha wanajenga uzio, ikiwa ni  sambamba na kuweka mageti yatakayowarahisishia wananchi kufikia ofisi hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali. Huku akiwapongeza TBA, pamoja na  wakandarasi mbalimbali walioshiriki katika ujenzi huo.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa aliongeza kuwa “watanzania wengi wamenufaika kwa kuwepo kwa miradi hii, kwa vile ujenzi huu  na mingine inayoendelea imesaidia kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania”.

Naye, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema kuwa huduma mbalimbali zinaendelea kuimarishwa katika mji huo wa Serikali ikiwemo ujenzi wa barabara ambapo Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARULA) na Halmashauri ya Jiji wanaendelea na ujenzi wa kilomita 18 kati ya kilomita 39 zi;izopo  ndani ya mji huo wa Serikali.

[caption id="attachment_41450" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenister Mhagama, akiwasilisha ripoti ya mwenenendo wa ujenzi wa majengo mbalimbali ya wizara kwenye Mji wa Serikali Ihumwa, Dodoma mbele ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. Leo Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa majengo hayo na ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.[/caption]

Maeneo mengine ni usafiri na mgahawa, ambapo Halmashauri zimeshaanza zoezi la kukamilisha viwango vya nauli kutoka maeneo mbalimbali kuelekea mji wa  Serikali.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Wazee na Wenye Ulemavu, Mhagama, alisema kuwa “tayari Wizara ya Fedha imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya pamoja na ununuzi wa gari la wagonjwa litakalotoa  huduma kituoni hapo”

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa wizara yake kupitia TANESCO itafunga transfoma yenye ukubwa wa KVA 300 katika mji huo wa Serikali  ili kuweza kutoa huduma ya  umeme kwa wizara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupitisha nyaya za umeme ardhini badala ya nyaya hizo kuonekana juu ya ardhi.

Ujenzi wa Mji wa Serikali ni moja ya agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambapo alizitaka wizara zote kujenga ofisi zake katika mji huo na kuhamia mapema iwezekanavyo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma zote za Serikali katika eneo moja.

[caption id="attachment_41451" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, akifurahia jambo na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya wizara mbalimbali kwenye Mji wa Serikali Ihumwa, Dodoma. (Picha na Idara ya Habari-MAELEZO)[/caption]

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi