Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uchaguzi Mdogo wa Kata Sita Kufanyika Mei 19 Mwaka Huu
Apr 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage akifafanua jambo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari (Hawapo Pichani)

Na. Idara ya Habari-NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye Kata sita (6) zilizopo kwenye Halmashauri sita (6) katika Mikoa sita (6) ya Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesema Jijini Dar es Salaam leo (Jumanne 09.04.2019) kwamba uchaguzi huo utafanyika tarehe 19 Mei mwaka huu.

Akisoma taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume, Jaji Kaijage amesema kwamba fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya  tarehe  15  hadi tarehe 19, Aprili mwaka huu.

Aidha Mwenyekiti  huyo wa Tume amesema kwamba uteuzi wa wagombea pia utafanyika tarehe  19, Aprili mwaka huu na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20, Aprili hadi tarehe 18 Mei mwaka huu.

Alifafanua kwamba uchaguzi katika kata hizo, utafanyika sambamba  na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki

“Tume inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na Maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo,” alisema Jaji Kaijage.

Awali Jaji Kaijage alisema kwamba maamuzi ya kutangaza uchaguzi kwenye kata hizo yamefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye  dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wazi wa nafasi hizo.

Alisema kwamba nafasi hizo wazi zimetokana na vifo vya Madiwani watano (5) na mmoja (1) kujiuzulu.

Kata hizo ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Mikocheni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Mvuleni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi na Manda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi