Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tusiishi kwa Mazoea, Tupambane na Korona
Mar 18, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu-Maelezo

Maamuzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona kwa kufunga shule zote za awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu, vya kati na vya chini, ikiwa ni pamoja na kusitisha mikutano, semina, warsha na shughuli za kijamii jambo ambalo ni msingi wa kuthibiti ugonjwa huo.

Maamuzi hayo yalitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokutana na Waandishi wa Habari ofisini kwake Magogoni Jijini Dar-es-salaam kwa siku mbili tofauti na kusisitiza taifa kuwa na tahadhari ya ugonjwa wa Korona ambapo mpaka sasa Tanzania ina ongezeko la wagonjwa wawili na kufanya idadi ya wagonjwa kufikia watatu.

Akinukuu taarifa yake ya matokeo ya Maabara Kuu iliyotolewa na Arusha na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy, Mwalimu Waziri Mkuu amesema “Tayari kuna wagonjwa wawili mmoja ni Mjerumani ana miaka 24 yupo Zanzibar amepata maambukizi na sasa yupo kwenye uangalizi pia kuna Mmarekani mwenye miaka 61 ambaye yupo Dar-es-salaam na yeye yuko katika uangalizi maalum hivyo tunaongezeko la wagonjwa wawili”.

Alitoa wito kwa Watanzania na kuwaomba kuwa makini lakini kutokuwa na taharuki na kuchukua hatua stahiki na kuendeleza kusitisha baadhi ya shughuli ambazo sio za lazima kama vile kupunguza msongamano na mkusanyiko isiyo ya lazima.

Aidha, ametaka huduma za usafirishaji ziendelee zikiambatana na utoaji wa elimu ya ugonjwa huu, lakini watu wakishajaa kwenye viti dereva aondoe gari badala ya kubaki na tabia ya kujaza kupita kiasi inayohatarisha afya za wasafiri. Pia, shughuli za masoko maduka na huduma kama hizo bado zitaendelea kutolewa kama kawaida ili wananchi wasikose huduma ya kujipatia mahitaji ya lazima kama vile chakula bila kujihusisha na mikusanyiko isiyo ya lazima.

“Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi wanashauriwa wasitishe safari hizo”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kinga ni bora kuliko tiba na katika maisha hakuna mazoea ya kuishi na ugonjwa hususan kama huu ambao unasambaa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu aliyepata maambukizi hayo kupitia jasho au majimaji yanayomtoka katika viganja, pua, mdomo mafua na anapopiga chafya na kukohoa.

Aidha, mtu yeyote anaweza kuambukizwa anapopeana mikono na mgonjwa wa korona, kukumbatiana au kugusa majimaji au jasho, mafua hivyo ni jambo la msingi kuchukua tahadhari ili kujikinga na maambukizi na kuzuia kusambaza kwa watu wengine katika maeneo yetu.

Jambo la msingi ni kubadilisha aina ya mtindo wa maisha ambao Watanzania wamezoea kuishi kama vile kupeana mikono, kukumbatiana, kupiga chafya bila kufunika mdomo, kujaza kupita kiasi kwenye magari yanayotoa usafiri wa umma na watu kupumuliana kwa karibu sana na kupakana jasho wakati wa msongamano huo.

Ipo mifano hai ambayo tunaona baadhi ya nchi kama Italia, zinapambana katika hali ya taharuki kutokana na idadi kubwa ya watu kuambukizwa ugonjwa huu, pia kusababisha vifo kadhaa ambavyo vinapelekea nchi hiyo kuchanganyikiwa zaidi na kuona imechelewa kuchukua hatua za dhati ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huu hatari..

Akielezea hatua nyingine zilizochukuliwa na serikali ili kuthibiti ugonjwa huo Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imesitisha Michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili na kuitaka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuziandikia barua Taasisi zake kutekeleza agizo hilo.

“Tunatambua vyuo vya elimu vingetakiwa kufanya mitihani mwezi Mei mwaka huu namuagiza Waziri wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo Profesa Joyce Ndalichako afanye marekebisho ya muhula wa mitihani yao kama vile tulivyomuagiza kufanya marekebisho kwenye mihula yao katika shule za sekondari za kidato cha sita”, amesisitiza Waziri Mkuu.

Suala la msingi kabisa kwa Watanzania ni kubadilisha mfumo wa maisha na tabia ambazo zimezoeleka katika jamii zetu, mfano kusalimiana kwa kushikana mikono. Aidha, serikali itaendelea kuwa makini na wageni wanaoingia nchini kutoka nje kwa kuhakikisha wanakaguliwa na kupimwa kwa makini kuhakikisha kuwa hawana maambukizi ya ugonjwa wa Korona.

Pia, tahadhari inahitajika kwa wafanyabiashara wa maduka ya dawa ambao wamechukulia tatizo hili kwa kujinufaisha kwa kupandisha bei bidhaa muhimu zinazotumika katika kujikinga na ugonjwa huu kama vile dawa za kusafisha mikono (sanitizer) na kuvaa barakoa (mask)

kupandisha bei ya bidhaa hizo na kudhoofisha vita dhidi ya mapambano hayo. Pia, wananchi wawe waangalifu na bidhaa wanazouziwa kama ni sahihi na sio feki na muda wa matumizi ya vifaa na dawa husika.

Watanzania wametakiwa kuwa makini wanapomuona mtu mwenye dalili za ugonjwa au binafsi unapopata dalili za ugonjwa wa Korona kama vile kuwa na homa kali, mafua, kuumwa na kichwa, kupumua kwa shida tafadhali piga simu namba zifuatazo ambazo hutatozwa gharama yeyote; 0800-119124, 0800-110125, na 0800-110037.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi