Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tunaendelea Kuwekeza Kwenye TEHAMA - Mhe. Silaa
Oct 15, 2024
Tunaendelea Kuwekeza Kwenye TEHAMA - Mhe. Silaa
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa akikagua mabanda ya maonyesho wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 8 la TEHAMA Tanzania ((8th Annual Tanzania ICT Conference) linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC )jijini Dar sa Salaam leo tarehe 15 Oktoba 2024.
Na Grace Semfuko - Maelezo

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kufanya maboresho ya kisera, kisheria na kitaasisi pamoja na kujenga uwezo kwa Watanzania lengo likiwa ni kuifanyia Tanzania kuwa sehemu ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Mhe. Silaa ameyasema hayo leo Oktoba 15, 2024 wakati akifungua kongamano la nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Tanzania, linaloendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema Wizara anayoiongoza pamoja na majukumu mengine, imepewa jukumu la kusimamia sera ya TEHAMA 2016 ambayo inalenga kukuza matumizi ya TEHAMA nchini.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kasi kubwa katika TEHAMA ambayo ndio nguzo kuu ya kufikia Uchumi wa Kidijitali Duniani, dunia hivi sasa ipo katika kipindi cha Mapinduzi ya Nne, Tano na Sita ya viwanda ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji kwa kiasi kikubwa inakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA." Amesema Mhe. Silaa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Abdulla Mohammed Khamis Abdulla amesema kuwa Kongamano hilo la nane lina sura ya kimataifa ambapo washiriki kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi wameshiriki,  tutashuhudia utoaji wa tuzo ya kimataifa ambapo Tanzania imekuwa mwenyeji kwa kuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa mashindano yaliyoandaliwa na Umoja wa Afrika kuhusu masuala ya Akili Mnemba na Roboti.

"Lengo la Kongamano hili ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya TEHAMA watakaojadili masuala yanayohusu TEHAMA ili kuhamasisha matumizi ya TEHAMA nchini. Kauli mbiu ya Kongamano hili ni kutumia uwezo wa Akili Mnemba na Roboti kwa mapinduzi ya kiuchumi na kijamii.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Prof. Leonard Msele ameeleza kuwa walianza Kongamano la kwanza la TEHAMA mwaka 2017 na wamekuwa wakijadili masuala ya uchumi wa kidijitali na mengine lakini kwa sasa wameamua kujikita katika eneo la Akili Mnemba na Roboti kwa sababu ndio eneo linalojadilliwa zaidi duniani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi