Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, amesema ni muhimu kwa Watanzania kufahamu hatua za maandalizi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akibainisha kuwa Dira hiyo imebeba matumaini ya wananchi na inalenga ustawi wa pamoja, jambo linalotokea mara chache katika historia ya Taifa.
Akizungumza leo Februari 1, 2026 jijini Dodoma kuhusu masuala ya utekelezaji wa Dira ya 2050, Dkt. Msemwa ametoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kufuatilia kwa karibu mijadala ya Bunge inayohusu mipango ya Taifa.

“Naomba kutoa wito kwa wananchi na wadau wote kufuatilia uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Taifa wa Miaka Mitano 2026–2031 pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, yatakayowasilishwa Bungeni Februari 2, 2026 na Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo,” amesema Dkt. Msemwa.
Ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Mipango imeandaa nyenzo tatu muhimu zitakazowezesha utekelezaji wa Dira ya 2050, ambazo ni kukamilika kwa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa miaka 25, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026–2031) pamoja na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka wa fedha 2026/2027.

Sambamba na hilo, Dkt. Msemwa amesema tume hiyo imeandaa Muongozo wa Upangaji wa Mipango ya Taifa, na imefanya semina na viongozi wa halmashauri zote 184 nchini, wizara, idara na taasisi za umma kwa lengo la kujadili muongozo huo na kufikia uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayozingatia Dira ya 2050.
Aidha, amesema Tume ya Taifa ya Mipango ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini (National Planning Management Information System – NPMIS), unaolenga kuleta mageuzi katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango kwa kuzingatia matokeo ya kazi na uwajibikaji, ambao unatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Julai 2026.