Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema Mahakama ni ushirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa, sambamba na jukumu lake la kusimamia haki nchini.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini, ambapo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Nchimbi amesema Mahakama si chombo cha utoaji haki pekee bali ni nguzo muhimu ya ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.

“Mahakama si tu chombo cha kuimarisha utoaji wa haki nchini bali ni ushirika muhimu katika safari ya maendeleo ya Taifa,” amesema.
Ameeleza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Mchango wa Mahakama katika Ustawi na Maendeleo ya Taifa” imebeba ujumbe unaoonesha wazi kuwa Mahakama ni muhimili unaochangia maendeleo ya kiuchumi, ustawi wa jamii pamoja na kudumisha amani ya Taifa.
Balozi Nchimbi ameongeza kuwa Mahakama ni moja ya mihimili mitatu ya Dola, mingine ikiwa ni Serikali na Bunge, na kusisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu wa mihimili yote mitatu, kila mmoja ukitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.
Amesema Mahakama ina jukumu la kuhakikisha haki inapatikana kwa wote bila upendeleo, hofu wala uonevu wa aina yoyote, huku Bunge likiwa na jukumu la kutunga sheria na Muhimili wa Utendaji ukiwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Serikali.

Akizungumzia utendaji wa Mahakama, Balozi Nchimbi amesema mwaka 2025 Mahakama ilishughulikia mashauri ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 50, ambapo mashauri yenye thamani ya shilingi trilioni 13 yalisikilizwa na kuamuliwa kati ya mwezi Oktoba hadi Disemba 2025.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuchochea ustawi wa maendeleo ya Taifa, kwa lengo la kujenga taifa lenye amani, uchumi jumuishi na uimara wa kudumu.