Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika uendeshaji wa Reli ya TAZARA pamoja na reli za mijini, hatua inayolenga kuimarisha usafiri wa reli nchini na kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 1, 2026 jijini Dodoma kuelezea utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100 za muhula wa pili wa uongozi wake amesema Serikali imefanya maboresho ya uendeshaji wa Reli ya TAZARA, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uendeshaji wa kusuasua.
Profesa Mbarawa amesema kupitia maboresho hayo imekamilisha majadiliano na wawekezaji na kusaini mkataba wa ufufuaji na uboreshaji wa reli ya TAZARA Septemba 29, 2025 kati ya Serikali za Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).

Aidha, Profesa Mbarawa amesema Wizara hiyo imeendelea kuboresha mikakati ya uendelezaji na uendeshaji wa reli nchini, ambapo ndani ya siku 100, Upembuzi Yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa ya mijini katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma umekamilika.
Amebainisha kuwa hatua hiyo imewezesha kupatikana kwa fedha za msaada kwa ajili ya usanifu wa kina, hatua itakayofungua njia ya utekelezaji wa mradi huo unaolenga kupunguza msongamano wa usafiri wa umma na kuongeza tija katika miji mikuu ya kiutawala na kibiashara nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kujitegemea kifedha kuanzia mwezi Desemba, 2025, baada ya kwa zaidi ya miaka 13 kutegemea ruzuku ya mishahara kutoka Serikalini yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 13 kila mwaka. Kwa sasa, gharama hizo zitagharamiwa kupitia makusanyo ya ndani ya shirika.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha siku 100, Kampuni Tanzu ya TRC ijulikanayo kama Tanzania Railway Limited (TANRAIL) imeanzishwa. Kampuni hiyo inalenga kufanya uwekezaji na biashara kwa niaba ya shirika ili kuongeza mapato, na inamilikiwa kwa asilimia 100 na TRC. Uanzishwaji wake unatarajiwa kuongeza ufanisi na mapato ya shirika hilo.

Vilevile, amesema uendeshaji wa Reli ya Kisasa (SGR) na Reli ya Mita (MGR) umeendelea kuwa wa mafanikio makubwa. Katika kipindi cha siku 100, shirika limesafirisha abiria takribani 838,870, ambapo asilimia 89 walitumia SGR na asilimia 21 MGR.
Kwa upande wa mizigo amesema tani 85,735 zilisafirishwa katika kipindi hicho ambapo pia huduma ya SGR imefanikisha usafirishaji wa viongozi, watalii kuelekea hifadhi za taifa kama Mikumi, Ruaha na Udzungwa, wafanyabiashara, wananchi pamoja na makundi ya wanafunzi waliokuwa katika likizo kwa ajili ya shughuli za kielimu na utalii.