Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uhuru wa Mahakama Usitumiwe Kuficha Uzembe
Feb 02, 2026
Uhuru wa Mahakama Usitumiwe Kuficha Uzembe
Makamu wa Rais Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akisisitiza kuwa uhuru wa Mahakama ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba pamoja na sheria za nchi, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya sheria nchini katika viwanja vya mahakama jijini Dodoma
Na Baraka Messa-MAELEZO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewaagiza Majaji na Mahakimu nchini kuhakikisha uhuru wa Mahakama hautumiki kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini, akisisitiza kuwa uhuru wa Mahakama ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia Katiba pamoja na sheria za nchi.

“Kamwe uhuru wa Mahakama usitumike kama kichaka cha kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki,” amesema Balozi Dkt. Nchimbi.

Ameeleza kuwa Majaji na Mahakimu wanapaswa kutekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika Ibara ya 107A (2) (a)–(e) na Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo zinabainisha misingi ya uhuru wa Mahakama, uadilifu, uwajibikaji na haki kwa wote.

Makamu wa Rais amesema anatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha utoaji wa haki kupitia maboresho ya mifumo ya kazi pamoja na utungaji wa kanuni mbalimbali zinazosaidia usikilizaji wa mashauri ya madai na jinai kwa ufanisi zaidi.

Amebainisha kuwa kanuni hizo zimechangia kupunguza mlundikano wa mashauri, kuongeza uwazi katika mwenendo wa kesi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama, hivyo kuifanya Mahakama kuendelea kuwa nguzo muhimu ya haki na utawala bora nchini.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha uhuru wa Mahakama ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuchangia ustawi wa maendeleo ya Taifa.

 Vilevile, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama katika ujenzi wa miundombinu, kuimarisha rasilimali watu, kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama pamoja na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi, hususan kupitia mpango wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi