Tume ya TEHAMA kuanzisha kituo cha Ubunifu (Softcentre) Zanzibar, vinne vya Kanda katika majiji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Tanga, Lindi na Mbeya kwa ajili ya kuendeleza kampuni changa za TEHAMA na kuendeleza kituo cha Dar es Salaam ili kukuza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa za TEHAMA na kukuza uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Dkt. Nkundwe Mwasaga wakati akieleza kwa Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Tume hiyo na mafanikio yake leo Agosti 25, 2023 jijini Dodoma.
“Kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT refurbishment and assembly centre) na kuwezesha mafunzo maalum ya TEHAMA kwa wataalam kukuza na kuendeleza ujuzi wa TEHAMA nchini,” alisisitiza Dkt. Nkundwe.
Akifafanua, amesema hadi sasa Tume hiyo imeshasajili wataalam wa TEHAMA 1,600 wanaohudumia nchi nzima ikiwa ni moja ya hatua za kukuza sekta hii muhimu kwa uchumi na ustawi wa wananchi.
Akieleza mafanikio ya Tume hiyo amesema kuwa ni pamoja na Kampuni mbalimbali zimeweza kutengeneza mitaji mikubwa na zinafanya kazi nchi nyingi duniani hali inayaochangia kukuza ajira na uchumi.
Mafanikio mengine ni pamoja na kutengeneza mfumo jumuishi utakaounganisha usajili na uendelezaji wa wataalam na wabunifu TEHAMA nchini (ICT human capital development system): lengo la mfumo huu ni kutambua bunifu na kupanua wigo wa ukuzaji wa wabunifu na bidhaa na huduma za TEHAMA zinazozalishwa Tanzania na hivyo kukuza pato la Taifa na kuongeza fursa za ajira kupitia TEHAMA na maendeleo ya kidijitali duniani.
Akieleza vipaumbele vya mwaka 2023/2024 Dkt. Nkundwe amesema ni pamoja na kuanzisha kituo cha kutengeneza na kuboresha vifaa vya TEHAMA (ICT Refurbishment and Assembly centre), kuwezesha uanzishaji wa vituo vya majaribio vya ubunifu TEHAMA (District ICT Startups Innovation hubs) katika Wilaya 10.
Sanjari na hayo, Tume itaendelea kufanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA nchini na kufanya tathmini ya kitaifa ya hatua za utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya TEHAMA, kuratibu na kuandaa matukio ya kuvutia uwekezaji na kutangaza masoko ya bidhaa za TEHAMA ndani na nje ya nchi.
Hatua nyingine za mafanikio ni kushirikiana na washirika wa maendeleo na kampuni za kimataifa katika kuendeleza bunifu za TEHAMA ikiwemo kuwezesha utengenezaji wa bidhaa za TEHAMA hapa nchini.
Pia, Dkt Nkundwe ametaja mafanikio mengine kuwa ni kujenga kituo cha Artificial Intelligence kwa ajili ya kuendeleza wataalam wa TEHAMA, kuwezesha mafunzo maalum ya wataalam wa TEHAMA 500 ili kukuza na kuendeleza ujuzi wa TEHAMA nchini na kukuza soko la bidhaa na huduma za kampuni ndogondogo “startup” kwa kushiriki maonesho na makongamano yanayohusu fursa za startups duniani.
Kuratibu na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa utekelezaji wa Sera ya TEHAMA na kufanya tafiti za kuweza kufanya maboresho ya sera kulingana na mabadiliko ya teknolojia, kujenga metaverse studio kwa ajili ya kutengeneza maudhui ya metaverse na pia kuboresha maudhui ya mitandao na kufanya tafiti za maendeleo ya TEHAMA kwa kila wilaya, kuanzisha Kituo cha Resilience Academy hapa nchini.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeamua kuwekeza kwa nguvu kwenye Tanzania ya Kidijitali chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo msimamizi mkuu unafanywa na Tume ya TEHAMA.
Hili ni jambo kubwa kwani fedha nyingi imewekezwa kwa ajili ya kuboresha TEHAMA nchini kwani shughuli mbalimbali kwa sasa duniani zinafanyika kwa njia ya kidijitali ikiwemo huduma za malipo mabalimbali, huduma za afya za matibabu, uzalishaji, kilimo, uchimbaji wa madini.