Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tume ya Madini Yaja na Mikakati Mipya Ukusanyaji Maduhuli
Oct 30, 2023
Tume ya Madini Yaja na Mikakati Mipya Ukusanyaji Maduhuli
Kamishna wa Tume ya Madini, Prof. Abdulkarim Mruma
Na Mwandishi Wetu

Kamishna wa Tume ya Madini, Prof. Abdulkarim Mruma amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2023 ikiwa ni kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023-2024, tume imeidhinisha maombi mapya ya leseni za madini 7,596 ikiwa ni asilimia 100 ya maombi yaliyowasilishwa kama mkakati wa kuendelea kutoa fursa zaidi za uwekezaji katika Sekta ya Madini, wananchi kunufaika na Serikali kupata mapato yake.

Prof. Mruma ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2023 kwenye kikao cha tume jijini Dodoma chenye lengo la kupokea na kujadili taarifa za utendaji wa tume kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Makamishna wa Tume, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na Menejimenti ya Tume ya Madini.

Amesema kuwa, kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa wananchi kwenye uwekezaji katika Sekta ya Madini kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kupitia ziara, makongamano, warsha na maonesho mbalimbali sambamba na kuongezeka kwa kasi ya uchakataji wa maombi ya leseni mbalimbali za madini.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo akielezea hali ya utekelezaji kwenye eneo la ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023 kamati yake ilipokea mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini 234 ambapo mipango 232 ilipitishwa baada ya kukidhi vigezo.

Amefafanua kuwa elimu kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini imeendelea kutolewa sambamba na matumizi ya  mfumo wa usimamizi wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa jamii na wadau wa madini nchini.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Mhandisi Yahya Samamba akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli amesema kuwa kati ya kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023, Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 184.53 na kusisitiza kuwa tume kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa imeendelea kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 882.12 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023-2024 linafikiwa.

Ameeleza kuwa katika kipindi husika, ulifanyika ukaguzi wa migodi, mitambo ya uchenjuaji wa madini na utoaji wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali nchini hasa kuhusu usalama kwenye shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.


“Pia tume ilifanya ukaguzi ili kutathmini eneo lililopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la topesumu kwenye migodi au mitambo ya uchakataji wa madini katika miradi ya  Green Pacific Investment Limited katika Kijiji cha Mbangala, Wilaya ya Songwe Mkoani Songwe, Adam Thomas Mungirwa katika Kijiji cha Mtakuja, Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Kampuni ya Mwaloni Limited iliyopo Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara; Hexad Company Limited na Nyati Gold Mine katika Mkoa wa Geita na Msalala Gold Mine Ltd iliyopo Kahama, Mkoani Shinyanga,” amesisitiza Mhandisi Samamba.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesisitiza umuhimu wa kufuatilia madeni ya leseni za madini ambazo hazijalipiwa na watumishi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Tume.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi