Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TSC Yatakiwa Kufanya Tathimini ya Wazi Zoezi la Upandishwaji Madaraja kwa walimu
Sep 21, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwansdishi wetu - MAELEZO, DODOMA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli amewataka Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)  kufanya tathimini ya wazi ya zoezi la upandishwaji wa madaraja kwa walimu uliofanyika hivi karibuni ili kufahamu kama kuna uwepo wa rushwa ili hatua za kisheria zichukuliwe

Mweli ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi ya Kamati za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Wilaya kwa Kanda ya Kati.

Ameeleza kuwa, pamoja na zoezi hilo kufanyika kwa ufanisi zipo changamoto zilizojitokeza ambapo baadhi ya walimu kulalamika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji kutoa upendeleo kwa baadhi ya walimu ambao hawakuwa na sifa za kupanda vyeo huku wenye sifa wakiachwa.

“Unapokuta mtumishi asiye na sifa ya kupandishwa daraja kadhalika mwenye sifa ya kupanda daraja ameachwa ni lazima tupate majibu, hivyo viongozi mnapaswa kutekeleza wajibu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma kwani sifa za mtumishi kupanda daraja tunaangalia kazi, nidhamu na muda uliokaa katika utumishi”, amefafanua Mweli.

Aidha, ametoa wito kwa Viongozi   hao kuzingatia weledi katika majukumu yao ili kuweza kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya rushwa.

Vilevile amesema kuwa, TAMISEMI    imekusudia kuanzisha kituo maalumu cha huduma kwa wateja kwa lengo la kuwasaidia walimu nchini kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo. 

“Uwepo wa kituo hiki cha huduma kwa mteja kitasaidia walimu wetu kuwa na Mawasiliano ya karibu baina yao na Viongozi wa tume na hii itasaidia kupunguza muda mwingi wanaotumia katika kufuatilia changamoto zao”, amefafanua Mweli.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi