Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA Yavuka Lengo Makusanyo ya Kodi
Mar 12, 2025
TRA Yavuka Lengo Makusanyo ya Kodi
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 12, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Lilian Lundo – MAELEZO

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema katika kipindi cha miezi nane kuanzia mwezi Julai 2024 hadi Februari 2025, TRA imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.20 sawa na ufanisi wa asilimia 104 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 20.42 ambao ni ukuaji wa asilimia 17 ukilinganishwa na kiasi cha shilingi trilioni 18.6 kilichokusanywa  kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita 2023/24.

Bw. Mwenda amesema hayo leo Machi 12, 2025 wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.

“Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la shilingi trilioni 9.28 ambalo ni ukuaji wa asilimia 78 ukilinganisha na kiasi cha shilingi trilioni 11.92 kilichokusanywa kipindi cha mwezi Julai 2020 mpaka Februari 2021, kabla ya Mhe. Rais kuingia madarakani,” amefafanua Bw. Mwenda.

Ameendelea kusema kuwa, katika miaka minne ya Mhe. Dkt. Samia akiwa madarakani, makusanyo ya kodi yanayokusanywa na TRA yameongezeka kwa asilimia 78 kutoka shilingi trilioni 11.92 hadi shilingi trilioni 21.20.

Bw. Mwenda amesema kuwa, TRA imerahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wateja kwa kusogeza huduma za kikodi karibu na wananchi ambapo jumla ya ofisi mpya 40 zimefunguliwa katika maeneo ambayo awali hayakuwa na Ofisi, pamoja na kukarabati na kujenga ofisi 41 kuanzia ngazi za Mikoa, Wilaya, Vituo vya Ukaguzi (check- points) pamoja na ofisi za mipakani.

Aidha, mamlaka hiyo imejiwekea mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa inaendelea kukusanya mapato ya kutosha kwa lengo la kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo na kuimarisha huduma za jamii kwa watanzania.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo yote ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usimamizi wa kodi nchini na kuendelea kujenga na kuimarisha mifumo ya kodi za ndani na forodha, IDRAS na TANCIS inayosomana na mifumo mingine ili kurahisisha shughuli za kiuchumi nchini na kuongeza ulipaji kodi wa hiari pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi ili watekeleze majukumu yao kwa uadilifu na weledi

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi