Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limewezesha ujenzi wa vyoo bora kwa shule ya Msingi Kivinje yenye jumla ya wananfunzi 1320 iliyopo katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi. Akiongea wakati wa kukabidhi mfano wa hundi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyoo hivyo Meneja Mawasiliano wa TPDC Bi. Marie Msellemu ameweka wazi kuwa TPDC inatambua kuwa inawajibika kwa jamii ambayo inaendesha shuhguli zake mbalimbali na hivyo maendeleo ya jamii hizo ni suala la msingi kwa Shirika hilo.
“Sisi kama Shirika la Umma tunaowajibu kurudisha sehemu ya kile tunachopata kwa jamii zetu hizi ili kuweza kuboresha maeneo mbalimbali ya huduma haswa Afya, Elimu, Maji na utawala bora na hivyo ujenzi wa vyoo bora kwa wanafunzi wa Shule hii ya Kivinje inaangukia katika maeneo yote mawili ya elimu na afya.”
Alisisitiza kuwa suala la vyoo bora kwa wanafunzi ni muhimu sana haswa katika kuwapa faraja na kujiamini zaidi wawepo shuleni na hivyo kupelekea umakini zaidi katika masomo yao ambapo huwafanya wafanye vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Aidha akielezea maendeleo ya ujenzi wa vyoo hivyo, Bi Msellemu aliwahimiza Watendaji wa shule hiyo pamoja na Kamati ya ujenzi kuongeza kasi ya ujenzi wa vyoo hivyo ambavyo kwa sasa vilitakiwa kuwa vimekamilika kwa asilimia kubwa ili kuepuka kipindi cha mvua kubwa ambayo inatarajiwa kunyesha katika mwezi ujao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mfano wa hundi hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa Ndugu Ramadhani Hatibu alisema, ameridhishwa namna ambavvyo TPDC inavyoshirikiana na Halmashauri hiyo katika kusaidia katika uboreshwaji wa huduma mbalimbali za jamii.
Kaimu Mkurugenzi anaeleza zaidi “kwakweli TPDC mmekuwa mstari wa mbele katika kutushika mkono sisi kama Halmashauri ya Kilwa katika maeneo mbalimbali ambapo katika kumbukumbu zetu zinaonyesha mmefanya mengi tu yakiwemo mchango mlioutoa kawa ajili ya uboreshwaji na ujenzi wa maabara katika Shule zetu za Sekondari, ujenzi wa nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari ya Songo Songo, usambazaji wa huduma ya maji kwa Kijiji cha Songo Songo pamoja na Shule ya Sekondari Songo Songo pamoja na uendeshaji wa zoezi la upimaji wa afya na kukabidhi vifaa vya upimaji wa afya katika Kijiji cha Songo Songo”
Akiweka msisitizo Mkurugenzi huyo aliongezea kuwa “leo hii tunapokabidhiana rasmi kiasi cha milioni 16 lakini pia tunapokagua kwa pamoja utekelezaji wa ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi Kivinje inazidi kuleta faraja na matumaini katika uhusiano tulioujenga miaka mingi iliyopita na hivyo kwanza ni himize Kamati ya Ujenzi wa Shule hii kuhakikisha ujenzi huu wa vyoo unatekelezwa kwa kasi na weledi ili kutendea haki thamani ya pesa ambayo TPDC wametoa kwa ajili ya uboreshwaji wa shule yetu ili watoto wetu wawe na mazingira rafiki ya kujisomea ambayo yatapelekea ufaulu mzuri kwenye mitihani yao.“
Aidha akisoma taarifa ya ujenzi wa vyoo hivyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kivinje Ndg. Ngabuba alieleza kuwa, “Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 1320 kati yao wakiwa Wasichana 696 na Wavulana 624 na jumla ya Walimu 17 ambao kwa ujumla wetu tulihitaji kuwa na vyoo bora situ kwa kujisitiri lakini pia kuhakikisha suala la afya bora linazingatiwa na hivyo basi kwa kubahatika kupata msaada ktuoka TPDC kwakweli sasa tunaenda kuwa na vyoo bora ambavyo vitasaidia wanafunzi wetu kuwa na amani na kujiamini zaidi wawepo shuleni hapa”
“Kwakweli ujenzi umechelewa tofauti na ilivyopangwa nahii ni kutokana na mambo mbalimbali ya kiutawala na kiutaratibu lakini pia uhaba wa seruji ulitokea katika kipindi cha mwezi Juni lakini hivi sasa tuna ahidi kundelea na ujenzi kwa kasi na ufanisi zaidi ili tufikie thamani halisi ya pesa ambayo Shirika letu la TPDC limetoa” aliongezea Mkuu huyo wa shule.